Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Kenan Sawala leo tarehe 30 Machi 2025 amemuapisha Rachel Stephen Kasanda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi ambae amechukua nafasi ya Bw. Lauteri John Kanoni ambae uteuzi wake ulitenguliwa mapema wiki hii.
Kanali Sawala amempongeza Mhe. Kasanda kwa kuaminiwa tena na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwatumikia wananchi kwa nafasi ya Ukuu wa wilaya.
“Leo umeapa na umekabidhiwa Katiba, uilinde na kuitetea; pia umekabidhiwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwani ni chama kinachosimamia Serikali kutekeleza majukumu.” Alieleza Kanali Sawala
Aidha Kanali Sawala amemtaka Mkuu huyo wa wilaya kufanya mikutano ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kutembelea miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kutuma taarifa za utekelezaji kila mwezi.
Mhe. Kasanda pia ametakiwa kusimamia suala la elimu na kuhakikisha watoto walioandikishwa wanaripoti shule, kutokomeza utoro na kuhakikisha hali ya upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi. Huku akitakiwa kusimamia utekelezaji wa afua za lishe ili kuondokana na utapiamlo.
Akiwa kama Mwenyekiti wa Usalama wilaya, Mhe. Kasanda ametakiwa kusimamia usalama wa raia na mali zao ikiwa ni pamoja na kudhibiti biashara za magendo hususan maeneo ya mipakani.
Mwakilishi wa Kamishna wa maadili, Bi. Esther Lemther Laizer amemtaka Mkuu huyo wa wilaya kuzingatia Haki.
Mhe. Rachel Kasanda amewahi kuwa Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa mwaka 2014 na baadae kuwa Mkuu wa Wilaya ya Katavi na Magu kwa nyakati tofauti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.