Zainabu Mnyahi Nanchenda.
Maisha ni kupambana. Maisha ni kukazana. Neno moja la kimakonde linalobeba maana yote hiyo ni Tutumbame. Kwa asili ya wamakonde wanaopatikana mkoa wa Mtwara jitihada kubwa za Tutumbame huelekezwa katika kilimo cha korosho.
Pamoja na jitihada hizo zipo kaya ambazo kutokana na sababu mbalimbali zimejikuta ziko katika hali ya umasikini. Hawa wameingizwa katika Mpango wa Kunusuru kaya maskini (TASAF).
Moja ya vijiji vinavyonufaika na mpango huo mkoani Mtwara ni kijiji cha Tandika kilichoko Wilayani Tandahimba. Kijiji hiki ambacho uchumi wake unategemea zaidi kilimo cha korosho kina kaya 325. Kaya kumi kati ya hizo zimetambuliwa kuwa ni maskini na kuingizwa katika mradi wa TASAF.
Pamoja na kwamba mradi wa TASAF unatekelezwa mkoa mzima, Kijiji cha Tandika ni mfano mzuri kwa vijiji vilivyofanikiwa kujikomboa kwa kutegemea fedha za TASAF
Mwandishi wa Makala hii Evaristy Masuha alifunga ziara katika kijiji hicho na kujionea jinsi walengwa hao ambao wengi wao ni vikongwe wanavyonufaika na Mpango huo. Hapa anasimulia hali aliyoishuhudia.
Mtu wa Kwanza kuonana naye hapa kijijini alikuwa ni Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho Silla Ernest Jonsi ambaye alianza kwa kuelezea Jinsi walengwa hao walivyokuwa kabla ya mwaka 2014 mradi wa TASAF ulipoanza kutekelezwa. Anasema hali yao kimaisha haikuwa nzuri kabisa. Wote walikuwa wakiishi kwenye nyumba za nyasi huku wakipambana na mvua nyakati za masika hali ambayo ilikuwa ikileta usumbufu kwao. Sehemu kubwa ya pato lao ilikuwa likielekezwa kubadilisha nyasi za nyumba kabla ya masika.
Anaendelea kwamba walengwa hao hawakuona fahari kuitwa masikini. Mtazamo huo ukawasukuma kuunda kikundi ambacho walikiita Tutumbame jina ambalo linalenga dhamira yao ya kupambana.
“Tutumbame ni neno la Kimakonde. Maana yake kwa Kiswahili ni Tukazane, tuongezee bidii, tuongeze juhudi. Hii ndiyo lugha kuu wanayoiongea walengwa wetu. Hawajui Kiswahili hivyo tutakusaidia kutafasiri”.
Jonsi ambaye anadai amekuwa mtendaji wa kijiji hicho kwa miaka 8 sasa anaendelea kuwa, Kwa vile wote walikuwa na matatizo makuu yanayofanana hasa tatizo la makazi, walikubaliana kupeana kila mmoja shilingi 10,000 kila wanapopokea fedha za kunusuru kaya masikini ambazo kwa kila kaya hupokea wastani wa shilingi 20,000 kila baada ya mieizi miwili. Waliomba uongozi wa kijiji uwasaidie kusimamia makubaliano hayo.
“Nashukuru kwamba makubaliano hayo tumeyasimamia na sasa kila mmoja anaelekea kutimiza ndoto zake”. Walengwa 8 kati ya 10 tayari wameshaweka bati nyumba zao huku watatu kati yao wakisubiri zamu yao kukamilisha makazi hayo”. Anasema Jonsi.
Baada ya Jonsi, Mlengwa wa kwanza kumtembelea alikuwa ni Zainabu Mnyahi Nanchenda mjane na mama wa watoto 3 na wajukuu kadhaa. Mnyahi alianza kwa kuiishukuru serikali kwa kuleta mpango wa TASAF kwani kabla ya kuingia katika mpango hakuwa na ndoto za kuishi kwenye nyumba ya bati.
Anasema kabla ya nyumba ya bati anayoishi sasa alikuwa na nyumba ya matofari ya tope ikiwa imeezekwa kwa nyasi. Nyumba hiyo ilianza kukwanguka kuta kutokana na kunyeshewa mvua hali ambayo ilimfanya aishi kwa taabu sana.
Zamu yake ya kupokea ilipofika alipokea jumla ya shilingi 120,000 na kununua bati 9. Aliendelea kwa utaratibu huo huo hadi alipokamilisha bati za nyumba. Akaezeka kwa usimamizi wa serikali ya kijiji. Sasa anapanga mipango yake ya maisha bila hofu ya usalama wa nyumba.
Mwingine ni Bibi Sofia Hussein Liumba anakadiria umri wake kufikia miaka 70. Anasema kabla ya kuanza utaratibu wa vikundi ulioanza mwaka 215 alikuwa akinunua bati moja moja kila alipokuwa akipokea fedha za TASAF. Anasema hali hiyo ilikuwa ikimuwia ngumu kwani alikuwa akihitaji kusafirisha bati moja kutoka Tandahimba umbarl wa zaidi ya kilometa 20 kwa gharama kubwa.
Baada ya kuanza kikundi aliweza kupata shilingi laki moja mara moja akanunua bati zilizokuwa zimepungua. Sasa anajivunia mafanikio hayo kwani ameezeka nyumba yake na sasa yuko kwenye nyumba bora.
“Bila TASAF ningekuwa bado naishi kwenye nyumba ya nyasi” anahitimisha Bibi Sofia.
Malengo yao kwa pamoja ni kuhakikisha wanaondokana na umasikini na kuweka misingi imara kwa watoto wao ili wasije wakaishia katika umasikini kama walivyo wao.
Akizungumzia malengo ya mpango wa TASAF Mratibu wa TASAF Mkoa wa Mtwara, Bibi Tabitha Kilangia anasema Mpango wa TASAF ni kuhakikisha walengwa wote wanajikomboa kutoka Umasikini hivyo walichokifanya wakazi wa Tandika ndicho kinachokusidiwa. amewaomba viongozi wa kijiji kuendelea kuwasimamia walengwa hao ambao wengi wao Vikongwe na elimu yao ni ndogo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.