Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameyaagiza mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoani Mtwara kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kuwasisitiza wadau wake kuweka mbele uzalendo na maslahi ya Taifa.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo leo katika mkutano wa Pili wa mwaka wa Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Mtwara uliofanyika katika ukumbi wa Boma na kusisitiza kuwa Serikali inatarajia kuyaona mashirika hayo yakiendeshwa kwa kuzingatia maadili, mila, na desturi, misingi ambayo amesema itayaweka katika nafasi salama.
“Ndugu washiriki wa mkutano huu, ni matumaini yangu kuwa mtaitumia fursa hii kujadili kwa kina mwenendo wa utendaji na changamoto zinazoyakabili mashirika yenu ili baadaye mje na mikakati mizuri ya utatuzi wa chanagamoto hizo” alisema Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
“Hivyo ni matarajio yangu kuwa miongoni mwa mikakati mtakayokuja nayo ni pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kushirikiana na Serikali kutekeleza mipango ya maendeleo, kutekeleza mipango hiyo katika maeneo ambayo Serikali haikuweza kufika pamoja na kuweka mfumo endelevu wa kubadilishana taarifa” aliongeza Kanali Abbas.
Aidha Kanali Abbas amesisitiza kuwa, katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Mkoa inafanya jitihada za kuzijengea taasisi hizo mazingira wezeshi ni vema zikaanza kujijengea uwezo wa kifedha kama njia ya kuondokana na utegemezi wa misaada ya wahisani jambo ambalo limekuwa likidhoofisha maendeleo ya taasisi hizo.
“Ni dhahiri kuwa utegemezi wa misaada ya fedha na rasilimali kutoka kwa wafadhili ni kikwazo cha maendeleo ya taasisi zenu, hivyo ninawashauri mnapotoka hapa nendeni mkaangalie uwezekano wa kuanzisha vyanzo vipya vya mapato kupitia misaada hiyo hiyo ili pindi wafadhili watakapositisha huduma muweze kujiendesha wenyewe bila hofu” alisisitiza Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kufungua mkutano huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Abdallah Malela alimweleza mgeni rasmi kuwa kutokana na viashiria vya baadhi ya taasisi kujihusisha na vitendo vinavyokiuka maadili, Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ililazimika kufanya uchunguzi na hatimaye kuzibaini na kuzichukulia hatua baadhi ya taasisi zilizohusika.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mashirika yasiso ya kiserikali Mkoani Mtwara Baltarzar Komba amesema kuwa, kwa sehemu kubwa uongozi umejitahidi kuzielimisha taasisi zisizo za kiserikali kuzingatia sheria na kusema kuwa endapo kuna taasisi itafungiwa kutokana na uvunjifu wa maadili wahusika wanatakiwa kujilaumu wenyewe.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.