MELI ya kwanza kubeba Makaa ya Mawe imewasili Bandari ya Mtwara kwa ajili ya kupakia tani elfu 33 za Makaa ya Mawe kwenda nchini India.
“APRILIA NASSAU”, Jina la meli hiyo yenye urefu wa mita 183 imewasili Oktoba 31 mwaka huu majira ya asubuhi na kupaki kwenye gati ya zamani huku ikitarajia kuondoka baada ya kukamilika kwa shughuli za upakiaji.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo la kupakia Makaa ya mawe hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti amesema kuwa Meli hiyo ni ya kwanza kwa Bandari ya Mtwara kuanza kusafirisha Makaa ya Mawe na wanatarajia kusafirisha angalau tani elfu 40 kwa kila Meli.
Gaguti alisema Makampuni mengine ya usafirishaji yameonyesha nia ya kuja katika Bandari ya Mtwara kuingia kwenye biashara hiyo ya usafirishaji na kusafirisha Makaa ya Mawe hivyo upo uwezekano mkubwa wa kusafirisha zaidi ya tani elfu 40 kwa mwezi kutokea Bandari hiyo ya Mtwara.
“Kwa hiyo ni habari njema lakini pia tunafahamu umuhimu wa Bandari hii unakwenda kulinda miundombinu yetu ya nchi yetu lakini pia kupitia upande huu wa Kusini mwa Tanzania kutakuwa na ongezeko la mzunguko wa fedha, kutakuwa na ongezeko la ajira mbalimbali na hivyo kukuza uchumi wa Kusini lakini pia Mkoa wa Mtwara utaweza kukuza uchumi mkubwa katika nchini yetu”,Alisema Gaguti
Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Mtwara Mhandisi Juma Kijavara alisema kuwa, tayari wameshachukuwa tahadhari zote za kimazingira ikiwemo kuweka maturubai ili kupunguza chembe chembe za Makaa ya Mawe zinazoangukia Baharini au kuziondoa kabisa.
Pichani: Rc Marco Gaguti (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Bandari ya Mtwara Mhandisi Juma Kijavala
Hata hivyo amewatoa wasi wasi wasafirishaji ambao wanataka kutumia Bandari hiyo juu ya uwezo wa Bandari kwani zile tozo hazijapunguzwa kwa mzigo wa korosho tu bali ni kwa mzigo wowote utakaopitia Bandarini hapo kwahiyo ile asilimia 30 iliyopunguzwa kwenye tozo zao ni kwa ajili ya bidhaa yoyote inayopitia Bandarini hapo.
Katika hatua nyingine Meli ya mafuta imewasili katika Bandari hiyo yenye urefu wa mita 180 ambayo imepaki kwenye gati hiyo ya zamani ikiwa imeshusha mafuta zaidi ya lita Milioni 7 na gati hiyo kina chake ni kidogo kuliko gati mpya ambapo Bandari ina uwezo wa kufunga Meli kubwa zaidi ya Meli hizo mbali ambazo zimefunga Bandarini hapo kwa sasa.
“Kwahiyo uwezo upo na tunatarajia pia mizigo mingine kuendelea kuihudumia, tulikuwa tunaongelea kuwa tuna uwezo wa kufunga Meli nne kwa wakati mmoja leo mmeshuhudia Meli mbili zimefunga gati ya zamani na Meli mbili tuna uwezo wa kufunga gati jipya kwahiyo kama Bandari uwezo upo”,Alisema Kijavara
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Makaa ya Mawe ya Ruvuma Coal Limited Ryan Weinand alisema kuwa, Meli hiyo imakuja kwa majaribio kwani wanatarajia kuja kwa Meli nyingine Bandarini hapo wiki tatu zijazo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.