Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) wakipata maelezo juu ya Bandari ya Mtwara mara baada ya kuitembelea Bandari hiyo leo
Ubora wa Bandari ya Mtwara umeendelea kuonekana huku Zanzibar ikitafakari uwezekano wa kuitumia bandari hiyo kusafirisha mafuta. Hiyo inatokana na maboresho yanayoendelea katika bandari hiyo ikiwemo ujenzi wa Gati mpya yenye urefu wa mita 300 na kina cha mita 14.
Akizungumza na mwandishi wetu leo Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Mwalim Alli Mwalim amesema yeye pamoja na Bodi nzima ya ZURA wameamua kutembelea mkoa wa Mtwara ili kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo fursa ya matumizi ya Bandari hiyo katika kusafirisha mafuta kutoka nje ya Nchi.
Amesema kwa sasa wanaitumia sana Bandari ya Dar es Salaam lakini wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali ikiwemo kusubiri kwa muda mrefu kupakua mzigo hali ambayo imekuwa haiwapendezi wafanyabiashara.
Mbali na Bandari ya Mtwara Bodi hiyo ambayo itakuwa na ziara ya siku mbili Mkoani hapa itatembelea Kiwanda cha Saruji kcha Dangote, Kituo cha uzalishaji wa Nishati ya Umeme cha Mtwara, Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia Madimba pamoja na visima vya Gesi asilia vilivyoko Pwani ya Mnazi.
Amesema yako mengi yanayowavutia kujifunza kutoka Mtwara hasa ikizingatiwa kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati Zanzibar haina muda mrefu tangu imeanzishwa hivyo wanahitaji muda wa kujifunza kutoka sehemu mbalimbal nchini.
Awali akiwasilisha taarifa ya hali ya Bandari ya Mtwara, Mkuu wa Bandari hiyo Nelson Cosmas Mlali amesema maandalizi ya kuanza kusafirisha mafuta kupitia Bandari ya Mtwara ziko katika hatu ya mwisho. Lengo ni kuifanya Mtwara kuwa kituo cha kuhudumia mafuta kwa mikoa ya kusini.
Baadhi ya maboresho yanayoendelea hapo ni pamoja na ujenzi wa gati mpya yenye urefu wa mita 300 na kina cha mita 14. Aidha baada ya maboresho hayo bandari itakuwa na uwezo wa kuhudumia shehema ya tani 600,000 toka 400,000 za sasa.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Msaidizi anayehughulikia Huduma za Maji na Nishati mkoa wa Mtwara Cosmas Komba ameshukuru ujio wa wageni hao akielezea kuwa ni fursa nzuri ya wageni kujifunza mambo mbalimbali yanayoendelea mkoani Mtwara. amesema Mkoa unazo fursa nyingi ambazo ziko wazi kwa kila mwananchi hivyo wote wanaalikwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.