Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Norbert Kalembwe amewahakikishia wadau pamoja na wanainchi wanaoishi jirani na bandari hiyo kuwa shughuli zote zinazofanyika katika eneo hilo ikiwemo zile zinazohusisha kupokea na kusafirisha mizigo mbalimbali zinazingatia kanuni za afya na miongozo iliyowekwa kwa mujibu wa sheria kwa kuzingatia maslahi ya pande zote.
Kaimu Meneja Norbert Kalembwe ametoa kauli hiyo leo katika mkutano na waandishi wa habari bandarini hapo uliolenga kutoa ufafanuzi kuhusu mikakati ya bandari katika kuhakikisha inazingatia miongozo na kanuni zilizowekwa wakati wa kuhifadhi na kusafirisha mizigo michafu (dirty cargo) bila kuathiri afya za wanainchi na mazingira.
Pia Kaimu Meneja ameongoza kuwa kutokana na hofu na sintofahamu iliyokuwepo bandarini hapo kuhusu suala zima la uhifadhi na usafirishaji wa makaa ya mawe, tayari uongozi umechukua hatua za haraka zenye maslahi kwa pande zote.
Kalembwe amesema kuwa kwa kuzingatia maslahi na afya za watumiaji wote wa bandari hiyo na jamii inayozunguka; bandari imeanza kufanya maboresho kwa kutenga eneo la kisiwa mgao kuwa gati mbadala litakalotumika katika usafirishaji wa makaa ya mawe pamoja na mizigo michafu (dirty cargo) hivyo kupunguza hofu ya usafirishaji wa mizigo yote katika gati moja.
Aidha Kaimu Meneja Norbert Kalembwe amesisitiza kuwa maboresho hayo yataleta mapinduzi makubwa katika bandari ya Mtwara kwa kulifanya eneo lililokuwa likitumika kusafirishia mizigo mchanganyiko kutumika kuhudumia mizigo mingine bila hofu.
Halikadhalika Kalembwe ameongeza kuwa ili kuhakikisha bandari imepunguza athari za vumbi la makaa ya mawe kwa wananchi na wakazi wa maeneo jirani, uongozi wa bandari umeongeza vifaa maalum ikiwemo vinyunyizia mvuke (Spray canons), gari la kunyonya vumbi (Road sweeper truck), pamoja na nyavu za kupunguza kasi ya upepo kama njia ya kudhibiti athari zinazoweza kusababishwa na uhifadhi na usafirishaji wa mizigo ya aina hiyo.
Akihitimisha mkutano wake na wanahabari Kaimu Meneja Norbert Kalembwe ametoa wito kwa wadau wote wanaoitumia bandari ya Mtwara kuendelea kuitumia na kuiamini kwani ndio lango kuu la usafirishaji katika ukanda wa kusini huku akiwataka wakazi wanaoishi pembezoni na bandari kuondoa hofu kwani tayari serikali imeanza kutatua changamoto zote zilizokuwepo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.