Ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya Mhe. Hussein Bashe, Waziri wa kilimo mkoani Mtwara, leo tarehe 01/10/2024 amekagua eneo la mradi wa ujenzi wa kongani ya viwanda vya kubangua korosho liililopo Maranje, Halmashauri ya Mji Nanyamba aidha amezindua kiwanda cha TANECU cha kubangua korosho kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mhe. Bashe amemuagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho kuhakikisha wanajenga kiwanda cha kubangua korosho chenye uwezo wa kubangua tani 3,000 pamoja na kujenga maghala mawili yatakayoweza kuhifadhi tani 10,000 kila moja kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa korosho 2025/2026 katika eneo la Maranje.
“Niwahakikishie kuwa ruzuku za dawa za maji na sulphur zitaendelea kutolewa bure kwa wakulima wa korosho mpaka pale tutakapoona wakulima wameimarika.” Alieleza Mhe. Bashe
Waziri huyo wa kilimo amewahakikishia wakulima ongezeko la bei ya korosho kwa msimu wa 2024/2025 huku akisisitiza vyama vya vikuu vya Ushirika kuwalipa wakulima ndani ya saa 48 tangu kuuzwa kwa korosho.
“Mkulima anaeuza mazao kwenye chama chochote cha msingi tayari ana sifa ya kuwa mwanachama halali hivyo anaruhusiwa kugombea nafasi yoyote ya uongozi; tunataka Ushirika urudi kwa wananchi. Nimeshatoa maelekezo kwa Mrajisi na Mkuu wa Mkoa wasimamie kuhakikikisha mikutana inafanyika.” Aliongeza Mhe. Bashe
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuzidi kufungua fursa za kuinua uchumi wa wananchi wa mkoa huo na kuahidi kuisimamia vema sekta ya kilimo ili izidi biashara.
Oct 1, 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.