Ikiwa ni mara ya pili ndani ya miezi mitatu ya mwaka 2025, leo tarehe 15 Septemba 2025 mkoa wa Mtwara umepokea tena jopo la madaktari bingwa 54 ambao watatoa huduma za afya katika vituo mbalimbali katika Halmashauri zote 9 za mkoa wa Mtwara.
Akipokea madaktari bingwa hao Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Benedict Ngaiza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mtwara amewataka wakawe chachu ya mapinduzi katika uboreshaji wa huduma za afya ngazi ya msingi hadi Taifa huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupata huduma za afya.
Ujio wa madaktari bingwa hao unalenga kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi, ili kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na changamoto za uzazi, kupunguza vifo vya watoto na watoto wachanga pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya waliopo kwenye vituo vya afya na hospitali za Halmashauri na Wilaya.
Jopo la madaktari bingwa hao linajumuisha madaktari bingwa wa magonjwa ya Wanawake na Ukunga (Gynaecologist), wa Watoto (Paediatrician), wa Upasuaji/ Bobezi wa mfumo wa mkojo (Urologist), wa Usingizi na Ganzi (Anaesthesiologist), wa Magonjwa ya Ndani (Physician), wa Kinywa na Meno (Dental & Oral Specialist) pamoja na Muuguzi Bobezi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.