Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI Naliendele) Dkt. Fortunus Kapinga amesema tunda la bibo linaweza kuwa fursa mpya kwa wakulima wa zao la korosho kujiiinua kiuchumi kwa kutengeneza mvinyo.
Akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Biashara Mkoa wa Mtwara amesema kwa muda mrefu taasisi hiyo imekuwa ikifanya utafiti wa zao la korosho na kugundua bidhaa mbalimbali ikiwemo mvinyo wa mabibo.
Aidha, ugunduzi huo mpya utamuwezesha mkulima kunufaika na mazao mengine ya korosho badala ya ilivyo sasa ambapo thamani ya korosho imekuwa ikionekana kwenye mbegu yake pekee. Aidha uzalishaji huo utaongeza usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi na hivyo kuiongezea serikali mapato.
Amefafanua kuwa teknolojia hiyo ambayo itakuwa ya kwanza hapa nchini inajibu hoja ya muda mrefu ya uongezaji wathamani ya zao la korosho kwa kutumia bidhaa nyingine zinzazotokana na zao hilo. Pia ni njia nzuri zaidi kwani inamsaidia mkulima kuepukana na changamoto ya utunzaji na usafirishaji wa mabibo mabichi.
“Wakulima hawana haja ya kuhofia utunzaji na usafirishaji wa mabibo kwani mabibo yaliyofanyiwa utafiti na kubainika kuwa na sifa hiyo ni yale yaliyokaushwa”. Amesema Kapinga.
Mazao mengine ya korosho yaliyofanyiwa utafiti kituoni hapo ni pamoja na nishati na Mafuta ya kuulia wadudu ambayo yanatengenezwa kutokana na maganda ya korosho, maziwa yanayotengenezwa kutokana na mbegu za korosho pamoja na siagi ya korosho.
Naye Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa amepongea hatua hiyo na kuwataka wananchi wa mkoa wa Mtwara kuchangamkia fursa hiyo. Amewataka wafanyabishara wa ndani wanaoshughulika na biashara ya korosho kuanzisha mashamba ili kuongeza uzalishaji. Aidha serikali iko nao bega kwa bega kuhakikisha wanafanikiwa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.