Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Dotto Biteko leo tarehe 10/09/2024 ametoa Leseni ya Uendelezaji wa kitalu cha gesi cha Ruvuma, eneo la Ntorya, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kwa kampuni ya Ara petroleum na Ndovu Resources kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC).
Akieleza faida zitakazopatika kutokana na leseni hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Ndg. Mussa Makame alisema mbali na kutumia gesi Kama nishati ya umeme pia wanatarajia kujenga kiwanda kidogo cha kuifanya gesi iwe kimiminika ambapo itatumika kwenye magari.
Mhe. Biteko amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyeruhusu leseni hiyo kutolewa kwani kwa mara ya mwisho leseni ya kuendeleza visima vya gesi ilitolewa mwaka 2006.
“Ni maagizo ya Mhe. Rais kuwa popote penye rasilimali na uwekezaji katika miradi mbalimbali basi wazawa wanufaike kwanza. Hivyo niagize kwenye mradi wa gesi TPDC ianze kurudisha hisani kwa jamii (CSR) pia isisitize wakandarasi wake kufanya hivyo.” Alieleza Mhe. Biteko
Aidha, Mhe. Biteko ametoa maagizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ambako miradi inatekelezwa kuhakikisha wanatenga kiasi cha pesa kutoka kwenye Ushuru wa Huduma (Service Levy) wanazopokea kutoka kwenye makampuni ili ziweze kutekeleza miradi ya maaendeleo badala ya kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu pekee.
Katika hatua nyingine Mhe. Biteko ameshuhudia utiaji saini Mkataba wa Maelewano (Memorandum of Understanding) baina ya TPDC na Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ambapo TPDC tayari imetenga kiasi cha shilingi Milioni 700 zitakazotumika kujenga kituo cha afya Dihimba ikiwa ni urudishaji wa hisani kwa jamii (CSR).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.