Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Mhe. Gelasius Byakanwa amesema kipaumbele chake cha kwanza hadi cha tatu kwa mkoa ni elimu.
Aidha mkoa utajenga shule kwa kutumia michango ya kuchangia huduma za jamii (CSR) itakayosaidia kutatua changamoto za wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kufuata shule, pia kuondoa tatizo la baadhi ya wanafunzi wanaorubuniwa na wazazi kufanya vibaya.
Byakanwa ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika kikao cha wawekezaji na wafanyabiashara wa mkoani hapa na kusema ili mambo yote yaweze kwenda sawa elimu ni muhimu.
Amesema mkoa wa Mtwara ulikuwa ukisuasua katika matokeo lakini kwa sasa umeanza kupiga hatua baada ya jitihada kubwa iliyohusisha wadau mbalimbali wa maendeleo.
“Nilipoingia hapa kwenye mkoa tulikuwa tunasuasua sana kwenye elimu, mwaka 2017 matokeo ya darasa la saba mkoa wa Mtwara ulishika nafasi ya 22 kati ya mikoa 26 lakini mwaka jana 2018 mkoa ni wanane katika mikoa 26 ya Tanzania, ni hatua kubwa,”amesema Byakanwa
Amesema katika matokeo ya darasa la nne pia mkoa ulishika nafasi ya nane kitaifa lakini changamoto iko katika matokeo ya kidato cha nne ambayo ilishika nafasi ya 25 kitaifa.
“Ukiangalia takwimu kiwango cha ufaulu kimeongezeka lakini nafasi ya mkoa kitaifa bado ni mbaya, kwanza tumeshuka..kwa mwaka 2017 tulikuwa nafasi ya 20 lakini mwaka jana tumekuwa nafasi ya 25,”amesema Byakanwa
Amesema zipo changamoto mbalimbali ikiwemo walimu na uhaba wa walimu lakini kama mkoa watakuja na mkakati kuendelea kukutana na walimu wa sekondari kuwekeana utaratibu kuona ni kwa namna gani wataongeza ufaulu kwa kidato cha nne kama ilivyo elimu ya msingi.
Mshiriki wa kikao hicho, Hasnein Murji amesema wazo la kujenga shule ni zuri kwani itasaidia watoto wa mkoa huo kupata elimu.
“Sisi ndio watu wa Mtwara ni lazima tushirikiane kwa pamoja kuondoa changamoto zilizopo katika elimu ili kupiga hatua, tukitoa michango yetu na shule ikakamilika tutakuwa tumeweka alama,”amesema Murji
Mkazi wa Mtwara Ally Sudi amesema “Inapendeza kuona mkoa umekuja na wazo la kujenga shule kubwa kwa ajili ya wanafunzi itawasaidia kuondokana hata na vile vishawishi ambavyo vilikuwa vikiwasababishia kukatisha masomo sababu ya ujauzito lakini wavulana na wao hawatakuwa tena watoro,”amesema Sudi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.