Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa( Mb) amesema serikali ya awamu ya sita tayari imeweka mikakati madhubuti ya kukuza sekta ya Kilimo nchini kama njia ya kumkwamua mkulima na kumfanya aondokane na dhana ya Kilimo cha mazoea.
Mhe Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo mjini Mtwara katika hafla ya Uzinduzi wa Ofisi za Benki ya Maendeleo ya Kilimo Kanda ya Kusini na kusema kuwa tayari serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 200 ambapo inatarajiwa kuona wakulima katika maeneo mbalimbali wananufaika na fursa hiyo.
Pia Mhe Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa kufuatia ujio wa benki ya TADB Mkoani Mtwara anatarajia kuona Kasi ya Maendeleo inaongezeka na kuwavutia wawekezaji mbalimbali kuwekeza mkoani hapa.
Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa serikali kwa kuthamini na kutambua umuhimu wa kuboresha sekta hii muhimu, tayari imeanza kuchukua hatua katika maeneo kadhaa yanayogusa sekta hiyo ili kuongeza tija.
''Ndugu wageni wote mlioshiriki katika hafla hii, napenda kuwahakikishia kuwa tayari serikali imeanza kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya wakulima, wafugaji pamoja na wavuvi" alisema Mhe Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Miongoni mwa maeneo ambayo Waziri Mkuu Majaliwa ameyataja kuwa serikali imeanza kuchukua hatua ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na usafiri wa anga.
Ndugu wageni waalikwa, viongozi na watendaji wote naomba nichukue fursa hii kuwathibitishia kuwa serikali ya awamu ya sita kwa dhati kabisa imedhamiria kumkwamua mkulima katika Kanda ya Kusini" alisisitiza Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa.
"Miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na kuongeza ruzuku ya pembejeo za Kilimo, ujenzi wa barabara ya kilometa 160 Kutoka Mnivata hadi Masasi, Maboresho ya Bandari ya Mtwara, ujenzi wa uwanja wa ndege Mtwara pamoja na ununuzi wa ndege kubwa ya mizigo jitihada ambazo ninaamini zikitumika kama ilivyokusudiwa zitaongeza tija katika eneo hili" aliongeza Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha Waziri Mkuu Majaliwa ameutolea Mfano mpango wa Mafunzo ya Kilimo kwa vijana unaojulikana kama Jenga Kesho iliyo Bora kuwa ni kielelezo cha jitihada za serikali kumkwamua kijana kupitia sekta ya Kilimo na kusema kuwa mpaka sasa zaidi ya vijana 800 tayari wamepata mafunzo kupitia mpango huo.
Kwa upande wa sekta ya uvuvi ambayo ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato kwa Wananchi wa Mkoa wa Mtwara, Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali imetumia kiasi Cha shilingi bilioni 34 kuwajengea uwezo vijana ili waweze kuendesha shughili zao za uvuvi kwa tija katika ukanda wa Kusini katika Bahari ya Hindi.
Kufuatia Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Benki ya TADB Mkoani Mtwara, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa amewataka wadau mbalimbali kuitumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi halikadhalika kukuza pato la Taifa.
Awali alimkaribisha Mgeni rasmi katika hafla hiyo naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande ameutaka uongozi wa Benki hiyo kuepuka urasimu katika mchakato wa kutoa Mikopo huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Newala akihimiza umuhimu wa kutoa Elimu ya Mikopo kwa wakulima.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameishukuru serikali kwa kuupatia Mkoa wa Mtwara fedha nyingi za maendeleo ikiwemo zinazogusa sekta ya Kilimo na kuahidi kuwa serikali ya Mkoa itahakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Ziara hiyo ya siku 6 ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) itaendelea tena kesho Julai 7, 2023 katika Halmashauri ya Manispaa- ya Mtwara Mikindani pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.