Wananchi wakiwasilisha ujumbe wao kwa Serikali wakati wa maonesho ya Nanenane Ngongo
Changamoto ya upatikanaji wa salfa kwa ajili ya zao la mikorosho kwa mikoa ya Mtwara na Lindi litafikia mwisho Augosti 20 mwaka huu. Kuchelewa kwa salfa hiyo inayotolewa bure kwa wakulima wa maeneo haya lilitokana na kuchelewa kwa mipango ya ununuzi ambayo kwa sasa inakwenda vizuri.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. Charles Tizeba wakati akiwahutubia mamia ya wananchi wa mikoa ya Kusini waliohudhuria kwenye maonesho ya wakulima kitaifa maarufu kama Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Ngongo vilivyoko Manispaa ya Lindi Mkoani Lindi.
Mheshimwia Tizeba alikiri kuchelewa kwa usambazaji wa pembejeo hiyo ambapo amesema amesema tani ambazo zimeshaingia katika mikoa ya Lindi na Mtwara hadi sasa ni zaidi ya tani elfu 16 huku tani 2100 zilizobaki zikitarajiwa kuwasili julai 20 mwaka huu. Amesema mahitaji ya mikoa ya Mtwara na Lindi ni zaidi ya tani elfu kumi na nane.
Ametaja baadhi ya changamoto zilizochelewesha usambazaji wa pembejeo hizo kuwa ni pamoja na tatizo la takwimu za wakulima halisi wa mikorosho na idadi ya mikorosho waliyonayo. Anasema takwimu hizo ambazo hupatikana kutokana na vyama vya ushirika zilionesha mahitaji salfa kwa mikoa hii miwili ni zaidi ya tani 18,000 jambo ambalo walilifanyia kazi na kuagiza kiasi hicho.
Zaidi ya tani kumi na sita alfu zimeshafika nchini na kugawanywa kwa wakulima. Bado tani 2100 ambazo zimeingia bandarini jana na zinatarajiwa kusambazwa muda si mrefu na hivyo tatizo la pembejeo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara litafikia mwisho.
Amezitaja baadhi ya changamoto kubwa zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa utoaji wa pembejeo bure kwa wakulima kuwa ni pamoja na wale waliokuwa wakinufaika na mfumo wa zamani ambao walikuwa wakiuza Salfa hiyo kwa bei ya juu kujiingiza kwa mbinu mbalimbali ili kuvuruga mfumo.
Pia wapo waliokuwa hawako katika mfumo ushirika wa vyama vya wakulima ambao baada ya utaratibu wa bure walijitokeza na kutaka kupata mgao. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri ameagiza watu wenye sifa hiyo wasipewe kwani hawakuwa katika orodha ya idadi ya salfa iliyoagizwa.
Ameitaja changamoto nyingine kuwa wapo watu ambao wamekuwa wakichukua mifuko ya pembejeo iliyokwisha tumika wanaweka salfa ziliozpitwa na wakati na kuiuza madukani. Ameagiza viongozi wote wanaosimamia suala hilo kuwa makini ili kuhakikisha watu hao hawafanikiwi.
Awali akielezea mikakati ya serikali katika kuwakomboa wakulima, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema serikali imeweka mikakati imara ya kumkomboa mkulima. Ametaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuondoa tozo zisizo za msingi ambazo walikuwa wakitozwa wakulima.
‘Kwa kutambua kuwa zaidi ya silimia 65.5 ya watanzania wanajihusisha na kujiajiri katika sekta ya kilimo, Ufugaji na Uvuvi tumeendelea kuweka mipango kabambe ya kuhakikisha sekta hizi zinakua na wananchi wanafaidika nazo’. Alisema Makamu wa Rais.
Moja ya mikakati hiyo ni pamoja na kupunguza ushuru wa mazao, uliokuwa unatozwa na serikali za Mitaa kutoka asilimia 5 hadi asilimia 3 kwa mazao ya biashara na silimia 2 kwa mazao ya chakula.
Hatua nyingine ni kupiga marufuku utozaji wa ushuru kwa mazao yanayosafirishwa kutoka halsmahsauri moja kwenda nyingine ambayo uzito wake hauzidi tani moja. Amesema hizo zote ni njia za kumkomboa mkulimwa wa Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.