Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Mhe. Andrey Avetisyan leo Septemba 8, 2025 amewasili mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo anatarajiwa kutembelea miradi ya maendeleo katika wilaya za Mtwara Mjini na Vijijini pamoja na Newala.
Katika salamu zake za ukaribisho, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala amemweleza Balozi Avetisyan kuwa serikali ya Mkoa inafungua milango kwa wawekezaji kutoka Urusi kuwekeza katika sekta viwanda vya kubangua korosho, uchumi wa bluu, nishati, kilimo na usafirishaji na kusisitiza kuwa serikali imeweka sera nzuri na rafiki zinazo walinda wawekezaji.
“Mhe. Balozi napenda kukuhakikishia kuwa serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini na kuuenzi uhusiano wa nchi zetu mbili uliodumu kwa miongo kadhaa, hivyo kupitia Mkoa wetu wa Mtwara naomba uwafikishie salamu ndugu zetu wanaotaka kuwekeza Tanzania wanakaribishwa sana, fursa ziko nyingi tutawapa ushirikiano” alisema Kanali Sawala.
Kwa upande wake Balozi Avetisyan ameipongeza serikali ya Tanzania kwa sera bora za biashara na uchumi hatua ambayo amesema inaishawishi serikali ya Urusi kuwahamasisha raia wake kuutembelea Mkoa wa Mtwara na kuwekeza katika fursa zilizopo.
“Mhe. Mkuu wa Mkuu wa Mkoa binafsi ninafurahi sana kutembelea Mtwara, nimesikia ukielezea fursa nyingi na nzuri katika sekta mbalimbali, naomba kuchukua fursa hii kukuhakikishia tuko tayari kushirikiana na nyinyi, katika sekta za ujenzi wa barabara, viwanda vya kuchakata mbolea na gesi,usafirishaji majini pamoja na kandarasi za ujenzi wa barabara, maeneo yote haya tuna wataalamu na teknolojia ya kisasa” alisisitiza balozi Andrey Avetisyan.
Kuhusu ushirikiano katika sekta ya elimu Balozi Andrey Avetisyan amesema serikali ya nchi hiyo hivi sasa imeongeza nafasi za wanafunzi wanaokwenda kusoma fani mbalimbali huku akiwataka wanafunzi wenye sifa kutoka Mtwara kuitumia fursa hiyo.
Katika siku ya kwanza ya ziara ya Balozi wa Tanzania nchini Urusi Mhe. Andrey Avetisyan mkoani Mtwara ametembelea bandari ya Mtwara, Kongani la viwanda vya korosho katika Halmashauri ya Mji Nanyamba pamoja ofisi za Bodi ya korosho mjini Mtwara.
Aidha Balozi Avetisyan amesema kuwa Ujumbe wake umevutiwa na mradi wa ujenzi wa Kongani la Viwanda vya kubangua korosho katika Kijiji cha Maranje katika Halmashauri ya Mji Nanyamba ambapo amesema wanakusudia kuitangaza fursa hiyo nchini Urusi ili iweze kuzinufaisha pande zote mbili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.