Simulizi hii inatoka kwenye kitabu cha ‘The Flags Changed at Midnight: Towards the Independence of Tanganyika’. Kimeandikwa na Michael Longford. kimechapishwa mwaka 2001 na MPG Books LTD.
Mwandisi wa kitabu hiki, Michael Longfold alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara wakati wa serikali ya kikoloni. Aliingia nchini mwaka 1951 akitokea Uingereza akiwa ni miongoni mwa maafisa ishirini waliosambazwa kwenye makoloni ya waingereza kote Afrika. Eneo lake la kazi lilikuwa ni Mtwara wakati huo ikiwa chini ya jimbo la Kusini. Pia aliwahi kuwa Katibu wa Gavana wa Tanganyika, Edward Twining. Alikaa Tanganyika kwa miaka kumi. Nafasi yake ya Ukuu wa Wilaya ya Mtwara ilikoma baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, akalazimika kurudi kwao Uingereza.
Anasimulia hali halisi ya mji wa Mtwara wakati huo na jinsi alivyoshiriki katika mambo mengi ya ujenzi wa koloni hili la Uingereza malengo makuu yakiwa ni kuhakikisha rasilimali inayopatikana katika mikoa ya kusini inanufaisha serikali yake.
Anaanza kwa simulizi ya Bandari ya Mtwara ambayo leo hii ina umuhimu mkubwa kwa wanamtwara na Tanzania kwa ujumla. Longfold ambaye analitaja jimbo la kusini kama ‘Cinderella Province’ (jimbo lisilojulikana) anaisikitikia serikali yake kwamba hawakuwaza vema katika uamuzi wao wa kujenga bandari ya Mtwara.
Anaanza kwa kukumbuka mazingira magumu aliyokutana nayo katika utekelezaji wa shughuli zake za Ukuu wa Wilaya ikiwemo kuhakikisha bandari ya Mtwara inawanufaisha waingereza walioijenga mwaka 1950.
Anasema lengo lililokusudiwa katika ujenzi wa bandari ya Mtwara halikufikiwa, Yeye akiwa mtekelezaji mkuu na msimamizi wa Wilaya ya Mtwara alikutana na changamoto nyingi ambazo zilitoa majibu ya wazi kwamba serikali yake (serikali ya Uingereza) haikufikiria kwa usahihi na wala hawakujipanga ipasavyo kuwezesha lengo kufikiwa.
Anasema wazo la ujenzi wa bandari lilikuwa limeshikiliwa kidedea na Waziri Mkuu wa Uingereza kwa Wakati huo, Clement Attlee mara baada ya chama chake cha Labour kuingia madarakani mwaka 1945. Serikali ya Clement ilikuwa imepitisha sheria mbalimbali ambazo zililenga kupambana na changamoto mbalimbali ikiwemo Sheria ya huduma ya Afya, Sheria ya Bima na sheria ya National Assistance Act ambazo zote ilikuwa ni utekelezaji wa taarifa iliyokuwa imetolewa na Sir William Beveridge ikilenga kuondoa matatizo ya maradhi, ujinga, utapiamulo na ukosefu wa kazi kwa waingereza.
Ili kupambana na changamoto zote hizo ndipo serikali ikaamua kuanzisha mashamba ya karanga taklibani acre milioni 3 kwa Tanganyika nzima. Hilo likaenda sambamba na sheria mpya ya majimbo ya nje. (The Overseas Resources Development Act).
Ili kuwezesha usafirishaji wa mazao ya karanga kutoka jimbo la kusini kwenda Uingereza serikali ikaona umuhimu wa kujenga bandari ya Mtwara.
Anasema kosa kubwa lililofanyika katika utekelezaji wa hilo ni kushindwa kuyasoma mazingira ya makoloni hasa jimbo ya kusini. Hilo likafanya mashamba yashindwe kufanya kazi na hivyo bandari nayo ikakosa kazi.
Kosa hilo lilianzia kwenye manunuzi ya vifaa vya kulimia kutoka kwenye mabaki ya zana za kivita ambazo zilitokana na vita ya pili ya dunia. Kwa mtazamo wake anasema serikali ilishindwa kufikiria zaidi iwapo vifaa hivyo vina sifa ya kufanya kazi za kilimo kwenye maeneo vinakopelekwa. walishindwa kupima iwapo wataalamu wa kuviendesha na hata usafirishaji wake kutoka huko ulaya hadi jimbo la kusini unawezekana kirahisi. Pia upatikanaji wa vipuri. Anatolea mfano kuwa suala la kubadilisha Mizinga na vifaru kuwa Matrekta lilikuwa ni suala gumu ambalo liliisumbua serikali wakati mradi miradi ya kilimo ikiendelea.
kwa ujumla mashamba ya karanga kwa mikoa ya kusini na bandari ya Mtwara havikuinufaisha serikali ya kikoloni zaidi ya kupoteza muda na gharama kubwa ya ujenzi na uanzishwaji wake. Bandari ya Mtwara ikawa haina kazi kwa muda wote wa utendaji kazi wa serikali ya kikoloni.
Hali ya Bandari baada ya uhuru.
Miaka 68 sasa tangu bandari hiyo kujengwa na miaka 58 tangu uhuru wa Tanganyika Bandari ya Mtwara imekuwa na umuhimu mkubwa kwa wanamtwara na Tanzania kwa ujumla. Bandari hii iliyojengwa ikiwa na uwezo wa kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka ghati yake ina Urefu wa Mita 385 na kina cha mita 9.5 (CD). Sasa imefanyiwa maboreshio mengi ikiwemo upanuzi wa ghati mpya yenye mita 300 ambayo ujenzi wake unaendelea.
Upanuzi huu unatokana na umuhimu wake mkubwa katika kusafirisha shehena ya Mizigo toka mikoa ya kusini. Miaka ya hivi karibuni bandari hii imefanya kazi kubwa wakati wa ujenzi wa viwanda vya saruji kikiwemo kile cha Dangote na Mtwara Cement.
Pia usafirishaji wa korosho kupitia bandari hii hasa baada ya serikali kuagiza usafirishaji wa korosho kutoka mikoa ya kusini upitie bandari ya Mtwara. Mfano Katika kipindi 2015/16 hadi 2017/18 jumla ya tani 544,184.908 zimesafirishwa na ziliipatia serikali shilingi 275,639,370,270.66
Aidha, Huduma ya mafuta ambayo ilikuwa ikipatikana kutokea bandari ya Dar es Salaam sasa mafuta hayo yanafikishwa mikoa ya kuisni kupitia bandari ya Mtwara.
Bado fursa ya kupanua kwa bandari hii ni kubwa kwani madini ya Kinywe (graphite) yaliyogundulika katika vijiji vya Namangale na Utimbula huko Lindi pamoja na Miji ya Chiwata na Chidya, Masasi Mtwara yanatarajiwa kusafiriswa nje ya nchi kupitia bandari ya Mtwara.
Wakati akitambulisha mradi huu kwa wadau mapema mwaka jana Katika Ukumbi wa Kagwa Lindi Msimamizi wa Kampuni iliyogundua Rasilimali hiyo Nachi Resource LTD, Godwin Nyero alisema hadi wakati huo walikuwa wamegundua tani milioni 416 katika maeneo hayo na makadirio yao watakuwa wakisafirisha tani 1,000,000 hadi 180,000 za malighafi hiyo kupitia bandari ya Mtwara.
Tukutane Next week ambapo Michael Langford atasimulia alivyokoswakoswa kutumbuliwa kwa sababu ya kuruhusu makao makuu ya Wilaya yahamie yalipo sasa kutoka Mikindani.
Evaristy Masuha
0788 437778, 0717,697205
jevaristy@yahoo.com
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.