Naibu Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Kaspar Kaspar Mmuya ameziagiza Halmashauri na Uongozi wa Mkoa wa Mtwara kuweka mikakati Madhubuti ya kukabiliana na maafa pindi yanapojitokeza sambamba kutoa elimu kwa wananchi hatua itakayosaidia kupunguza athari zake.
Mhe Mmuya ametoa agizo hilo leo katika kikao kazi maalumu kilichofanyika mjini Mtwara na kilicholenga kuandaa mpago wa kukabiliana na maafa katika ngazi mbalimbali maalumu kwa ajili ya mkoa wa Mtwara.
Naibu Katibu Mkuu Mmuya amesema kuwa kujitokeza kwa maafa katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchini ni jambo lisiloepukika na kwamba kutokana na athari zake kwa jamii na mazingira ikiwemo, Ofisi ya Waziri Mkuu tayari imeimarisha mifumo ya uratibu katika ngazi zote.
“Ndugu wanasemina, leo hii tunakutana hapa kuandaa mpango Madhubuti wa kukabiliana na maafa, ni matumaini yangu mpango huu utasaidia kupunguza vihatarishi kama vile mafuriko na vimbunga” alisisitiza Mhe Mmuya.
Halikadhalika Mmuya amesema kutokana na ongezeko la matukio ambayo yamekuwa yakisababisha maafa na kuathiri mifumo ya kawaida ya maisha, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP ililazimika kuunda kamati ambazo zimejadiliana na sekretarieti za Mikoa ya Lindi na Mtwara zikiwemo halamashauri ili kubaini vihatarishi na kupima utayari wake katika kukabiliana na matukio ya aina hiyo pindi yatakapojitokeza.
Naye Mkurugenzi Kitengo cha Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mumanga amesema kuwa asilimia 80% ya majanga yanasababishwa na baadhi ya mifumo ya maisha isiyo rafiki ikiwemo uharibifu wa mazingira unaochangia mabadiliko ya tabia nchi na kusisitiza kuwa jamii itakuwa salama endapo kutakuwa na mpango madhubuti wa kukabiliana na maafa katika ngazi zote.
“Wahenga wanasema ukishindwa kupanga basi elewa fika umepanga kushindwa, ndugu zangu nawaomba muitumie warsha hii kupendekeza mambo muhimu kwenye mpango huu yatakayokuwa dira ya kukabiliana na maafa katika mkoa wenu mkizingatia rasilimali mlizonazo” alisisitiza Meja Jenerali Mumanga.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara Abdallah Malela ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa miongozo na elimu ambayo imekuwa ikiitoa kwa watendaji na wataalamu ndani ya mkoa wa Mtwara na kuahidi kusimamia utekelezaji wa mpango huo pindi utakapokamilika.
Warsha hiyo ya siku moja imehudhuriwa na wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama za mkoa na wilaya mkoani Mtwara, wataalamu kutoka halmashauri na sekretarieti ya mkoa, viongozi wa dini pamoja na viongozi kutoka taasisi na mashirika binafsi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.