Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewaagiza viongozi pamoja na wataalamu katika ngazi ya Halmashauri kuweka mfumo nzuri utakaosaidia watendaji kuepuka mazingira yatakayosababisha kutengeneza hoja mpya na kuongeza kuwa utaratibu huo kwa kiasi kikubwa umekuwa ukichangia kudhoofisha maendeleo ya baadhi ya halmashauri.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao maalumu cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Newala ambapo amewataka wataalamu kwa kushirikiana na baraza la madiwani kuhakikisha wanabaini kwa haraka viashiria vya aina yeyote vinavyoweza kusababisha hoja na kuvidhibiti mapema kabla havijaleta athari.
“Mara nyingi hoja huwa hazitokei hivihivi tu, ni nyinyi wenyewe mnazitengeneza katika idara zenu lakini mwisho wa siku unakuwa mzigo wa taasisi nzima” alisema Kanali Abbas.
Aidha Kanali Ahmed Abbas Ahmed ametaja baadhi ya viashiria vinavyoweza kusababisha Halmshauri kupata hoja kuwa ni pamoja na kushindwa kufikia malengo ya makusanyo iliyojiwekea, kushindwa kudhibiti mifumo ya kukusanya mapato (POS) na kuruhusu ubadhilifu, kutosimamia vizuri utaratibu wa kurejesha mikopo ya vikundi pamoja na kukiuka matumizi sahihi ya mifumo ya manunuzi.
Halikadhalika Kanali Abbas pia amebainisha vitendo vingine vinavyoweza kuzalisha hoja kuwa ni kutumia mapato ghafi kabla ya kupelekwa benki, kushindwa kurekebisha kasoro za matumizi ya (POS) hasa pale mtumiaji anapotuma muamala kimakosa pamoja na utaratibu wa kuwakaimisha watumishi wenye sifa bila kuwathibitisha katika muda unaokubalika kisheria vitendo ambavyo amesema vimekuwa vikirudisha nyuma jitihada za Serikali za kuwahudumia wananchi na kutatua kero zao.
“Ndugu zangu Madiwani pamoja na wataalamu wetu nilikuwa najaribu kuwaonesha ni kwa namna gani tunaweza kutengeneza hoja sisi wenyewe, ninaamini mara baada ya kikao hiki mtakwenda kujipanga kuondoa dosari nilizozitaja katika baadhi ya maeneo" alisisitiza Kanali Abbas.
“Nendeni mkasimamie utekelezaji wa Sheria, Kanuni na taratibu, mtu yeyote atakayekiuka iwe ni kujihusisha na vitendo vya ubadhilifu wa mapato au kwa namna nyingine yeyote inayorudisha nyuma jitihada za halmashauri chukueni hatua” aliongeza Mkuu wa Mkoa.
Akiwasilisha ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2021/ 2022, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa nje Mkoa wa Mtwara Bi Janeth Kikoti amesema kati ya hoja 15 zilizopokelewa, hoja 7 zilifungwa na hoja 8 hazijafungwa zimesalia kwa ajili ya ufuatiliaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Newala Alhaji Kundya amesema Serikali ya Wilaya itahakikisha inasimamia kikamilifu mapungufu yote yaliyojitokeza ili Halmashauri hiyo iendelee kuweka rekodi ya kupata hati safi kama ulivyofanyika katika mwaka wa fedha uliopita.
Awali mapema asubuhi kabla ya kikao hicho Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed akiambatana na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Newala Alhaji Kundya alitembelea eneo la shimo la Mungu lililopo katika Halmashauri Mji Newala ambapo aliuahidi uongozi wa Wilaya hiyo kuwa Serikali ya Mkoa itahakikisha inatumia kila mbinu kulitangaza eneo hilo ili kupanua wigo wa utalii ndani ya Mkoa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.