Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wazazi na walezi kuepuka migogoro na mifarakano katika familia ili kupunguza wimbi la Watoto wanaoishi mtaani.
Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo katika mdahalo wa maandalizi ya kilele cha Siku ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi Mtaani uliofanyika katika Ukumbi wa VETA mjini Mtwara ambapo amesema katika siku za hivi karibuni baadhi ya wazazi wamejenga utamaduni wa kuzua migogoro inayosababisha ongezeko la talaka ambazo zimechangia ongezeko la watoto wa mitaani.
“Bila shaka nyote ni mashahidi wa matukio yanayoendelea katika jamii yetu, yaani huko ni purukushani tupu, leo mzazi huyo kamfukuza mkewe kesho mwingine anaomba talaka yaani kwa ujumla hali si shwari” alisema Waziri Gwajima.
Kufuatia hali hiyo Waziri Gwajima ameitaka jamii kuhakikisha inarejea katika misingi ya malezi kwa Watoto ambao ni kizazi cha kesho ili kuepuka vitendo vya mmomonyoko wa maadili ambavyo vinachangia ongezeko la Watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.
“Ndugu washiriki wa kongamano hili nimemsikia Mkuu wenu wa mkoa akisema kuna idadi ndogo ya watoto wanaoishi mtaani ambao hawazidi tisini, kwa ujumla hii ni habari njema, lakini naomba msibweteke endeleeni kuweka mikakati ya kuzuia ongezeko, kataeni mila na desturi kandamizi pia watumieni maafisa usawi wa jamii kutatua migogoro, halikadhalika jielimisheni kupitia maafisa maendeleo ya jamii kuhusu fursa za kiuchumi ikiwemo mikopo ya riba nafuu, kwa ujumla hatua hii itapunguza migogoro katika jamii” alisisitiza Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala amesema mkoa unaendelea kuweka mikakati endelevu ya kuondokana na tatizo hilo ikiwemo kutoa elimu kwa wazazi na walezi kupitia maafisa ustawi wa jamii kuhusu umuhimu wa kuwapa Watoto malezi bora sambamba na kuhakikisha unalinda haki za Watoto kama sheria inavyoelekeza.
Maadhimisho hayo yaliyobebwa na kauli mbiu “Imarisha ushirikiano kuzuia Watoto kuishi mtaani” yanafikia kilele chake hapo kesho mjini Mtwara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.