Wananchi wakifuatilia michezo iliyokuwa ikiendelea wakati wa Tamasha la MsangaMkuu Beach Festival 2018
Wahaya wanamsemo kwamba Akalezile enkonko tikagita. Tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi ni kwamba Kilichomlea Kuku hakimuui. Maana nyingine ni kwamba kitu kizuri kilichoandaliwa vizuri hakiwezi kukupa matokeo mabaya.
Msemo huu unanikumbusha jambo moja kubwa ambalo bado linazunguka kwenye kichwa changu takribani mwezi mmoja sasa.
Ni pale Desemba 30, 2018 eneo la Msangamkuu ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa aliwaongoza maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara katika uzinduzi wa Fukwe ya Msangamkuu. Uzinduzi huu ulitambulishwa kwa jila la “Msangamkuu Beach Festival 2018”, hii ikiashiria kwamba 2018 imeanza hivyo kuna miaka mingine ya tukio itafuata.
Nikiri kwamba uwepo wangu ndani ya mji wa Mtwara kwa takribani miaka 5 sasa nilikuwa sijawahi kushuhudia kusanyiko kubwa kama hilo likifanyika kando ya bahari. Hili ndilo linanipa msukumo wa tafakari na pongezi kwa wote waliobuni tukio hili.
Nianze kwa kuwapongeza waandaaji tukio hili kwa sababu fukwe hii imekuwepo tangu kuumbwa kwa dunia lakini hakuna aliyewahi kufikiria kama inaweza kutumika kuwakusanya wananchi wa ndani na nje ya mkoa wa Mtwara. Wakajumuika, wakashangilia na kufurahi pamoja.
Ni fukwe ambayo imekuwepo kwa muda Mrefu lakini hakuna aliyewahi kufikiria kama ni eneo ambalo wazee, vijana, akina mama, watoto, viongozi wa kisiasa na kidini pamoja na wageni mbalimbali wanaweza kukutana, wakacheza pamoja, wakaimba, wakashangilia, wakaongea na kunong’ona mambo mbalimbali ambayo pengine yangehitaji ziara maalumu ya kiofisi.
Ni fukwe ambayo kwa kuitazama utaamini iliwekwa makusudi kwa ajili ya kuwavuta watu kwa mapumziko ya baada ya kazi. Bahati mbaya ni eneo ambalo waliotanguliwa hawakuliona. Bahati mbaya sana sina msemo wa kimakonde katika hili lakini wakerewe wanasema Aho Babwenda Tibumela. (wanapouhitaji hauoti). Waswahili wakasema penye Miti hakuna wajenzi.
Waandaaji wa tukio hili wameamua kupingana na msemo huo. Sasa wanaamua kujenga baada ya kujiridhisha kuwa kila kinachohitajika katika ujenzi kipo.
Kwa hili nimpongeze Mkuu wa Mkoa na Viongozi wote wa mkoa wa Mtwara mlivyojichanganya na wanamtwara katika kulipamba tukio. Pongezi kwake bingwa wa kuogelea Mbunge wa Mtwara Vijijini Mhe. Hawa Ghasia kwa jinsi alivyovuta umati kwa uwezo wake wa kuogelea akiwa ameganda juu ya maji. Hongera Mhe. Byakanwa kwa jinsi ulivyojipambanua kupitia michezo mingi uliyoshiriki katika fukwe hiyo ikiwemo, mbio za kuchota maji, Soka la ufukweni, mazoezi ya ufukweni na kucheza mziki.
Mambo hayo ni ya kawaida sana lakini ujumbe mkubwa kwa jamii ni kwamba uongozi siyo kujionesha kwamba wewe ni wa pekee bali wewe ni kama wote wanaokuzunguka.
Vilevile nikupongeze Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa jinsi ulivyofanikisha zoezi hili kwa kuwatumia wananchi wenyewe. Taarifa iliyopo ni kwamba Uliunda kamati iliyojumuisha wananchi wa kawaida, wakazi wa Mjini Mtwara, ukawawekea mazingira ili waandae tukio hilo. Huu ndio Uongozi. Uongozi ni uwezo wa kufikiri na kuwashirikisha wengine katika utekelezaji. Hivi ndivyo walivyofanya viongozi wote waliofanikiwa.
kilichoko mbele yako sasa ni kuhakikisha unasimama katika msemo nilioutambulisha awali. Akalezile Enkonko Tikagita. Jambo hili ambalo umeliandaa vizuri lilete manufaa kwa wanamtwara. Kubwa ni kuhakikisha fukwe hii inatambulika kwa kila mtu ndani na nje ya nchi. Liwe eneo ambalo mataifa mbalimbali yatakuja, kujumuika na wanamtwara katika kufurahia mandhali ya mji wa Mtwara.
Najua hili ni moja ya agizo ambalo uliwapa kamati yako inayoongozwa na Swalah Said Swalah. Endelea kusimamia kuhakikisha ndoto zako zinafanikiwa. Sina shaka kwamba unaweza.
Nayakumbuka maneno ya Mhe. Ghasia wakati akizungumza na vyombo vya habari siku hiyo kwamba kuna fukwe nyingi zenye sifa tofauti tofauti ikiwemo ile ya Msimbati ambayo aliitaja kama fukwe pekee hapa nchini ambayo binadamu anaweza kuendesha gari kama anavyoendesha kwenye barabara ya lami. Fukwe zingine ni fukwe ya Mnazi ambayo ina urefu zaidi ya kilometa ishirini, fukwe ya Naumbu pamoja na ile ya Mgao.
Ninayo mifano mingi ya wageni ambao nimewapokea wakihitaji kupata eneo la kutalii, kupumzika. Mara nyingi watu wa aina hii kwa hapa mjini Mtwara wamekuwa wakielekezwa mji Mkongwe wa Mikindani. Si wote walio na mapenzi na kumbukumbu za kihistoria hivyo Msangamkuu utakuwa mbadala wa watalii wa mjini Mtwara.
Hatua iliyoko mbele sasa ni kuhakikisha maeno mengine mbalimbali ya hapa mjini yanatangazwa na na kuyaendeleza ili kuwavuta watu zaidi.
Watu wanapokuja kwenye fukwe ya Msangamkuu waende hadi Newala wakalione shimo la Mungu. Wajao Msangamkuu waende hadi Nanyumbu wakamuone nyani wa Mahinyo katika kijiji cha Chivilikiti ambaye ni maarufu kwa kuongoza watalii. Watu hawa tuwaongoze kutembelea Mbuga ya Lukwika Lumesule. Hawa waende hadi Luvula wakaione fukwe yenye mchangamweupe. wavione vinyago vya Wamakonde, Ngoma ya kimakonde na mengine mengi.
Niwapongeze tena wanamtwara, mmeianza vema hii hatua ya kuelekea Mtwara ya Utali
Mwandishi ni Evaristy Masuha. Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
0717697205
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.