Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema Mtwara na kisiwa cha Anjoun kilichopo Nchini Comoro wataendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ikiwemo Biashara, Elimu, Kilimo na Usafirishaji kama njia ya kudumisha uhusiano baina ya pande hizo mbili.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo wakati akimkaribisha Gavana wa Kisiwa cha Anjoun Mhe. Annis chamsidine pamoja na Ujumbe wa Madiwani ofisini kwake na kusema kuwa Comoro na Tanzania zimekuwa na mahusiano mazuri kwa muda mrefu hatua ambayo imechangia kuongeza kasi ya maendeleo baina ya pande zote mbili.
Kwa upande wake Gavana Annis chamsidine ameushukuru uongozi wa mkoa wa Mtwara kwa kufungua milango ya ushirikiano na kusema kuwa Comoro iko tayari kushirikiana kwa namna yeyote ili kuwasaidia wananchi wake kupata huduma muhimu kutoka mkoani Mtwara huku akiomba kutatuliwa changamoto zinazochelewesha utoaji huduma katika sekta za kilimo, biashara, elimu, na usafirishaji.
Gavana wa Kisiwa cha Anjoun Mhe. Annis chamsidine pamoja na Ujumbe wa Madiwani wake wako Mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo wanatarajiwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Bandari ya Mtwara, Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kusini, Mtwara pamoja na jengo la Halmashauri Mji Nanyamba na kujifunza utendaji kazi wa Halmashauri hiyo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.