Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega ameeleza msimamo wa Serikali wa kutomwongezea muda mkandarasi atakaechelewesha kukamilisha mradi.
Waziri Ulega ameyasema hayo leo tarehe 26 Mei 2025 alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara ya Mitesa-Masasi (km 60) yenye thamani ya Shilingi Bilioni 92 na Mnivata-Mitesa (km 100) yenye thamani ya Shilingi Bilioni 142 zinazojengwa kwa kiwango cha lami.
“Mkandarasi ongeza kasi ya ujenzi, msimu wa mvua unakaribia; ikiwezekana ongeza wafanyakazi wafanye kazi mchana na usiku, ongeza vitendea kazi. Serikali haitaongeza siku za mkataba na mkichelewesha tutaweza kuwadai fidia.” Alieleza Waziri Ulega
Aidha Waziri Ulega ameeleza kuwa ni matamanio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona uchumi wa wananchi mmoja mmoja ukikua.
“Niwatake wakandarasi kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakazi wa eneo husika, na kwa mahitaji yanayopatikana hapa mnunue kwao. Lakini pia mkumbuke kutekeleza miradi ya kurudisha fadhila kwa jamii (CSR) kama walivyokubaliana katika mikataba.” Alisema Mhe. Ulega
Katika hatua nyingine Waziri Ulega alidokeza kuwa Wizara ya ujenzi imepanga kununua taa 5,000 wastani wa taa 200 kwa kila mkoa, lakini mkoa wa Mtwara pekee barabara ya Mtwara-Masasi kupitia daraja la Mwiti zitawekwa taa 4,800.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.