NIMEWALETEA FEDHA NYINGI ZA MIRADI SIMAMIENI KWA UADILIFU-
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali ya awamu ya sita itaendelea na kasi ile ile ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kupeleka fedha katika maeneo mbalimbali nchini kama njia ya kutatua kero za wananchi.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo katika eneo la Magomeni mjini Mtwara wakati akiwa njiani kutoka Mkoani Lindi katika sherehe za siku ya Ukimwi duniani na kusisitiza kuwa serikali haitachoka kuwahudumia wananchi wake na itahakikisha maeneo yote yanayokabiliwa na changamoto zinazoathiri maendeleo ya wananchi yanafikiwa.
“ Ndugu zangu wanamtwara ni dhahiri kila binadamu ana wivu wa maendeleo, halikadhalika nyinyi mkiona mambo mazuri katika maeneo mengine bila shaka mtakuwa mnatamani mngepata nyinyi na hii ndio kawaida ya binadamu, mimi niwahakikishie serikali yenu inawajali itaendelea kutatua kero zenu kadri tutakavyofanikiwa” alisisitiza Rais Dkt Samia.
Halikadhalika Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameonya watendaji wanaofanya vitendo vya ubadhilifu katika baadhi ya halmashauri na kusisitiza kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikirudisha nyuma jitihada za serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi.
“Wakurugenzi tunawaletea fedha nyingi za miradi, lengo letu ni kuona fedha hizo zinatumika kama ilivyoelekezwa lakini kuna baadhi yenu wanazitumia kinyume, nisingependa tuje kulaumiana timizeni wajibu wenu mkiweka mbele maslahi ya wananchi na ya serikali” aliongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Aidha katika mkutano huo uliofanyika eneo la Magomeni mjini Mtwara, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alitoa fursa kwa mawaziri walioambatana naye kujibu kero zilizoibuliwa na wananchi pamoja na mbunge wa jimbo la Nanyamba Abdalla Chikota ikiwemo ufanisi mdogo wa bandari ya Mtwara, hali ya upatikanaji wa maji katika mji wa Mtwara pamoja na kushuka kwa bei ya korosho.
Akitolea ufafanuzi suala la kuongeza uwezo wa kusambaza huduma ya maji mjini Mtwara, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema mahitaji ya maji kwa mji wa Mtwara ni lita za ujazo milioni 22 ambapo kwa sasa mamlaka ya maji inazalisha kiasi cha lita za ujazo milioni 15.
“Mhe Rais tayari wizara imejipanga kuanza mradi mkubwa wa kuzalisha maji kutoka mto Ruvuma ambao utamaliza kabisa tatizo hilo” aliongeza Aweso.
Halikadhalika Waziri Aweso alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 19 kwa ajili ya kuboresha miundombinu chakavu ya maji katika mji wa Mtwara na hivyo kuongeza ufanisi katika swala zima la usambazaji wa maji kwa wakazi wa Mtwara na vitongoji vyake.
Akijibu hoja ya mbunge wa Nanyamba Abdalla Chikota kuhusu mwenendo wa biashara usioridhisha katika bandari ya Mtwara, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof Makame Mbarawa amesema baada ya kubaini hali hiyo Wizara kwa kushirikiana na uongozi wa bandari wameweka motisha kwa wadau wanaoitumia bandari hiyo hatua ambayo amesema imeanza kuonyesha dalili njema.
“ Mhe Rais serikali yako imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 159 katika mradi wa upanuzi wa eneo la maegesho ya meli katika bandari hii ambao tayari umekamilika, bila shaka hiki pia ni kivutio kingine kwa watumiaji wa bandari yetu kuleta meli kubwa za mizigo hatua itakayosaidi kuongeza kasi ya uchumi wa Mkoa wa Mtwara” alisisitiza Prof Mbarawa.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amekiri kuporomoka kwa bei ya korosho katika maeneo mbalimbali duniani na kusema kuwa wizara yake imepokea maelekezo ya mhe Rais na tayari imeanza kuyafanyia kazi.
“Mhe Rais kwa miaka mingi tumekuwa tukiuza nje kurosho ghafi isiyokidhi vigezo vya ubora, lakini kwa maelekezo yako mwaka huu tumeanza kuuza korosho iliyobanguliwa nchini Marekani ambapo tumeweza kusafirisha tani 7 kutoka Tandahimba, naamini huu ni mwanzo mzuri utakaoyavutia Mataifa mengi zaidi kununua korosho yetu” alisisitiza Waziri Bashe.
Kuhusu hujuma zinazofanywa na baadhi ya watu wasiohusika na kilimo cha zao la korosho ambao wakati wa ugawaji wa pembejeo wamekuwa wakinufaika na kuwaacha wakulima halali wakiumia, Waziri Bashe amesema Wizara yake hivi karibuni inatarajia kuanza zoezi la usajili wa wakulima wote kwa kuzishirikisha serikali za vijiji hatua ambayo amesema itaondoa wimbi la utapeli katika sekta ya kilimo cha korosho.
Awali Akimkaribisha Rais DKT Samia Suluhu Hassan Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abass Ahmed alimshukuru kwa kuupatia mkoa wake fedha nyingi za maendeleo katika miradi ya afya, elimu na kilimo na kusisitiza kuwa atashirikiana kikamilifu na safu ya watendaji wake katika kila ngazi kusimamia miradi hiyo kikamilifu.
Aidha Kanali Abass pia ameitumia fursa hiyo kumwomba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuuwezesha uwanja wa ndege wa Mtwara kupata jengo la kisasa la abiria ili kuufanya uwe na hadhi ya kimataifa.
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amemaliza ziara yake ya siku moja katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo akiwa Mkoani Lindi alihudhuria maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.