Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameziagiza taasisi zinazoshughulika na maswala ya Elimu pamoja na wadau kuiga mfumo wa kuboresha sekta ya Elimu unaotumiwa na MKoa wa Mtwara na kusema kuwa unaonyesha dira ya kuikomboa sekta ya Elimu.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Waziri wake Omari Kipanga aliyemwakilisha, imesema kuwa Serikali inatambua jitihada mbalimbali zinazofanywa na mkoa wa Mtwara katika kuboresha mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji hivyo itaendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kuboresha miundombinu na pia kuwawezesha watendaji.
Akikabidhi zawadi na vyeti kwa washindi katika Kilele Cha juma la Elimu mjini Mtwara, wakiwemo walimu, wanafunzi na wadau wa Elimu waliofanya vizuri katika mwaka wa masomo wa 2022/2023 Naibu Waziri Kipanga amesema utaratibu huo wa motisha utaongeza ari ya kufanya vizuri zaidi kwa walimu na wanafunzi mashuleni na hivyo kuufanya Mkoa kushika nafasi ya juu katika matokeo ya mitihani.
" Binafsi naomba nichukue fursa hii kuwapongeza sana kwa kubuni mfumo huu mzuri wa motisha katika Elimu, ninawaahidi nitakuwa Balozi wenu mzuri huko niendako kwa kuwahamasisha wadau mbalimbali kuwatembelea na kuiga mikakati mnayoitumia " alisema Naibu Waziri Kipanga.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed alimweleza mgeni rasmi kuwa baada ya kuanza kutumia utaratibu huo wa Motisha matokeo ya mitihani katika ngazi zote yameboreka tofauti na miaka iliyopita.
" Ndugu mgeni rasmi, kwanza kabisa ninaomba nichukue fursa hii kuipongeza serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuupatia Mkoa wetu fedha nyingi zinazogharimia sekta ya Elimu, sisi wanamtwara tunamuahidi tutasimamia kikamilifu sekta hii ya Elimu Ili tuweze kuandaa vijana watakaokuwa tegemeo la kesho" alisisitiza Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Abdallah Malela amewashukuru wadau waliofanikisha kupatikana kwa tuzo hizo zilizogharimu kiasi cha shilingi Milioni 143 yakiwemo magari 2 aina ya Noah, Pikipiki 13 ,baiskeli pamoja na fedha taslimu.
"Ndugu mgeni rasmi, naomba nizishukuru kwa dhati kabisa taasisi zote zilizochangia kufanikisha shughuli hii, bila kuwasahau wadau wetu wakuu TANECU na MAMCU, halikadhalika Benki ya CRDB pamoja na Dangote, tunawashukuru sana" alisema Katibu Tawala Abdallah Malela.
Katika tuzo hizo halmashairi ya Wilaya ya Newala imeibuka mshindi wa jumla ambapo imepata magari mawili aina ya Noah yenye thamani ya shilingi Milioni 50 huku walimu 8 wakizawadiwa Pikipiki na wengine fedha taslimu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.