Jamii mkoani Mtwara imetakiwa kutonyamaza na kutoa taarifa kwenye mamlaka za sheria zinazotoa haki pale wanapoona vitendo vya ukatili wa kijinsia bila kujali nafasi ya mhusika kwenye jamii.
Rai hiyo imetolewa na Mhe. Kanali Michael Mitenjele mkuu wa wilaya ya Tandahimba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara leo tarehe 10 Desemba wakati wa maadhimisho ya kampeni ya kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika wilayani Tandahimba.
“Ukatili wa kijinsia upo hata kwenye familia, lakini unakuta familia zinaamua kuyamaliza wenyewe; Mtu anakaa kimya ili kulinda heshima ya mtenda kosa lakini je, haki ya aliefanyiwa ukatili wa kijinsia inakuwa wapi? Tushirikiane kwa pamoja kupaza sauti, kutoa elimu ili kuwanusuru wahanga.” Alieleza Kanali Mtenjele.
Mkuu wa wilaya ya Masasi, Mhe. Lauteri Kanoni ameitaka jamii kuimarisha malezi ya watoto ili kuwa na jamii yenye kujali utu “Mwaka huu 2024 wana Mtwara Mungu ametujalia neema ya kutosha, mazao yetu ya korosho, ufuta na mbaazi yamepata bei nzuri; fedha hizi tuzitumie vizuri tusifanye ukatili wa kijinsia kwa watoto wetu kwa kusema hakuna pesa za kuwapeleka shule, tuwape haki yao ya kupata elimu.
Kwa mujibu wa taarifa za Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mtwara kuanzia Januari mpaka Oktoba 2024 watu 1,299 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia kati yao wanawake ni 1,009 na wanaume ni 290. Kwa upande wa watoto jumla ya matukio 713 yameripotiwa yakijumuisha utekelezaji wa familia, ukatili wa kingono, mimba za utotoni, ukatili wa kimwili; watoto wa kiume 374 na watoto wa kike 339.
Mashauri mbalimbali ya ukatili wa kijinsia mkoani Mtwara yamefanyiwa kazi; mashauri 1,759 yamemalizwa, 50 yapo mahakamani, 25 yametolewa hukumu,165 bado yapo hatua ya uchunguzi.
Kauli mbiu ya Kampeni ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia 2024 “Kuelekea miaka 30 ya Beijing chaua kutokomeza ukatili kijinsia”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.