JWTZ yasaidia ujenzi wa shule Nanyumbu.
Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa msaada wa vifaa vya ujenzi kwa Shule ya Msingi Michiga B iliyoko kata ya Michiga wilayani Nayumbu. Misaada iliyotolewa ni mifuko 200 ya saruji, mabati 100, Nondo 50 na shilingi 400,000 ambazo zitasaidia katika gharama za mchanga wa kujengea.
Akizungumza jana wakati wa kutoa msaada huo katika zoezi lililofanyika uwanja wa shule hiyo, Brigedia Jenerali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Brigedi ya Kusini, George Msongole amesema Jeshi limeguswa kutoa msaada huo kutokana na ukweli kuwa elimu ni moja ya njia kuu za ukombozi kwa mwananchi. Amesema aliahidi kutoa msaada huo mwanzoni mwa mwaka huu hatimaye ameamua kukamilisha ahadi.
Licha ya kutoa msaada huo Brigedia Msongole amesema jeshi litaendea kuwa karibu na shughuli nzima ya ujenzi wa shule hiyo na kwamba wameamua kumuweka mwakilishi wao mmoja ili kusimamia na kuhakikisha lengo lililokusudiwa linafikiwa.
Brigedia Msongole amesema jeshi la wananchi wa Tanzania limekuwepo kwa miaka 53 ambapo jana Septemba 1, lilikuwa likisherekea siku yake ya kuzaliwa na kwamba hiyo ni moja ya sababu kubwa ya kuunganisha sherehe za kuzaliwa kwa jeshi hilo na tukio la kukabidhi msaada huo.
Msongole ambaye juzi aliongoza maandamano kisha hafla fupi katika uwanja wa Mashujaa ulioko Mjini Mtwara ikiwa ni kukumbuka kuanzishwa kwa jeshi hilo miaka 53 iliyopita amesema anajivunia kuwepo kwenye mikoa ya kusini, hasa kutokana na ushirikiano mkubwa anaoupata toka kwa vipongozi wa mikoa ya Kusini. Amesema tangu amekuwepo hapa Mtwara amejifunza mengi hasa mshikamano mkubwa ulioko kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara.
Awali akisoma taarifa ya shule hiyo Mtendaji wa kijiji hicho Penina Frank Monjesa amesema ujenzi wa Shule hiyo ulitarajiwa kugharim shilinig 160,422,500 lakini kutokana na kujitolea wananchi katika kutumia nguvu zao, gharama zinatarajiwa kupungua hadi kufikia shilingi 80,000,000.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Halima Dendego ameshukuru Jeshi la wananchi wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa kusaidia ujenzi wa shule hiyo. Pia amekishukuru chombo cha habari cha Cloudz TV kupitia kipindi chao cha ‘Jicho la Mwewe’ kwa kuibua changamoto ya shule hiyo. Amesema chombo hicho kilitoa taarifa ya jinsi shule hiyo na changamoto kubwa ya utoaji wa elimu, wanafunzi walivyokuwa wakisomea kwenye mabanda ya nyasi jambo ambalo lililiibua hisia kwa jamii hatimaye makundi mbalimbali ya kijamii kujitokeza kusaidia ujenzi.
Aidha amemtaka mkuu wa Wilaya kuhakikisha anasimamia ujenzii huo ili ukamilike kwa haraka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.