Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala leo tarehe 24 Januari 2025 amezindua kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia (Samia Legal Aid Campaign) yenye lengo la kuhakikisha mifumo ya haki inaimarishwa na kwamba makundi yasiyokuwa na uwezo hususan wanawake na watoto wanaifikia haki kupitia huduma za msaada wa kisheria.
“Kampeni hii imekuwa ni mkombozi kwa wanyonge hususani wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili na kwamba inapunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko ya wananchi katika sekta ya sheria na kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani na katika vyombo vingine vya haki.” Alieleza Kanali Sawala
RC Sawala aliendelea kueleza kuwa kampeni hiyo inatekeleza falsafa ya 4R ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo ni Maridhiano (Rencoliation), Ustahimilivu (Resiliance), Mageuzi (Reforms), na Kujenga Upya Taifa (Rebuilding) ambazo ni misingi imara ya utawala wa sheria na utaoaji haki.
Kwa upande wake Mwakilishi wa naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndg. Abraham Mshamu alieleza kuwa kutakuwa na utolewaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa siku 9 katika Halmashauri zote tisa za Mkoa na katika ngazi ya Kata, Vijiji na Mitaa ambapo huduma zote zitatolewa bure.
Mwaka 2017 Serikali ilipitisha Sheria ya Msaada wa Sheria, Sura ya 21. Sheria hii imeazimia kuwasaidia wanyonge ambao hawana uwezo wa kifedha na hawana uelewa wa masuala ya sheria.
Huduma zitakazotolewa ni pamoja na elimu na ushauri katika masuala ya migogoro ya umiliki wa ardhi, mirathi, Ukatili wa Kijinsia hususan kwa wanawake na watoto, Matunzo ya watoto; na masuala ya ndoa.
Aidha, Wakala wa Usajili Ufilisi Udhamini (RITA) katika kampeni hiyo ya msaada wa kisheria ya mama Samia watatoa huduma za vyeti vya kuzaliwa, vifo na uandishi wa wosia huduma.
Kauli Mbiu ya Kampeni hii ni “Msaada wa Kisheria kwa Haki , Usawa, Amani na Maendeleo”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.