Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewataka wakulima wa korosho kuzingatia matumizi bora ya Kanzidata za kilimo cha zao hilo zitakazorahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kutoka katika taasisi mbalimbali.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo katika kata ya Naliendele, Manispaa ya Mtwara Mikindani wakati wa zoezi la kuhuwisha kanzidata za wakulima wa korosho na kusema kuwa hatua hiyo ni mkakati wa serikali wa kutatua changamoto za wakulima wa korosho.
"Ndugu wakulima mliopo hapa serikali yenu inatambua fika mnakabiliwa na changamoto nyingi, na hatua hii ni ishara tosha kuwathibitishia tayari imeanza kuhukua hatua" aliongeza Kanali Abbas.
Aidha Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema kuwa matumizi ya mfumo huo wa kisasa yataisaidia serikali kupitia Wizara ya kilimo kuzibaini changamoto za wakulima na kuzitatua kwa urahisi tofauti na siku za nyuma.
"Ndugu wakulima, mabibi na mabwana mliopo mahali hapa mara nyingi kumekuwa na taarifa nyeti kuhusu kilimo cha zao letu la korosho ambazo kimsingi mnatakiwa mzipate kwa wakati lakini kwa bahati mbaya kutokana na mazingira mmekuwa mkipata changamoto" alisema Kanali Abbas.
"Ukiangalia sasa hivi kuna taarifa nyingi mnazotakiwa kuzipata ikiwemo zinazohusu matumizi ya viwatilifu, taarifa kuhusu kuporomoka kwa soko la korosho na bei yake, zote hizi mtazipata endapo mtajisajiri katika Kanzidata hii" alisisitiza Kanali Ahmes Abbas Ahmed.
Aidha Kanali Abbas ameongeza kuwa Mkoa wa Mtwara umedhamiria kuongeza kiwango cha uzalishaji ifikapo 2025/2026 ambapo korosho ghafi inatakiwa kufikia tani laki 7, kiwango ambacho amesema kitafikiwa endapo wakulima wataelimishwa sambamba na serikali kutambua uhalali wa kila mkulima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Ndugu Aloyce Mwanjile amesema kwamba kanzidata ndio suluhisho la matatizo ya wakulima wa korosho kwa sasa na kwani itaifanya serikali itambue namba halisi ya wakulima na mahitaji ya mashamba yao.
"Ongezeko la uzalishaji ni lazima liendane na upatikanaji wa pembejeo sambamba na matumizi ya taarifa zilizomo kwenye kanzidata na leo ndio tumeanza rasmi" alisema Mwenyekiti Aloyce.
Wakati huohuo Bodi ya korosho imetumia fursa hiyo kuwatoa hofu wakulima ikiahidi kuwasajili wakulima katika kanzidata kwa wakati na kuwapatia elimu, zoezi litakalorahisisha upatikanaji wa taarifa zao wakati wowote zitakapohitajika.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.