Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Dkt.Leonard Akwilapo akikagua moja ya mabanda ya maonesho wakati wa kilele cha maazimisho ya wiki ya Elimu Kitaifa tukio lililoadhimishwa Mkoani Mtwara jana
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Dkt.Leonard Akwilapo amewataka wadau wote wa elimu kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto za elimu hapa nchini. Hayo amesema jana wakati akifunga Juma la Elimu Kitaifa lililofanyika shule ya Sekondari Mangaka iliyoko Wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.
Dkt. Akwilapo amesema changamoto za elimu ni nyingi hivyo zinapaswa kutatuliwa kwa ushirikiano wa kila mdau. Ameyataja baadhi ya masuala muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele kwa kipindi hiki kuwa ni pamoja na uimarishaji na usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji ambapo Walimu, Wadhibiti Ubora wa Elimu, Viongozi wa Halmashauri na wadau wote wa Elimu wanapaswa kuhakikisha wanatumia nafasi zao kuondoa changamoto hizo.
Katika sherehe hizo zilizoandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) Akwilapo amesema kwa sasa ufaulu wa shule zisizo za serikali hapa nchini zinaongoza. Siri kubwa ya ufaulu huo ni usimamizi mzuri jambo ambalo hata serikali inaweza iwapo kila mdau ataamua kuwajibika katika sehemu yake.
‘Kama serikali tunapaswa kuangalia na kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi. Walimu wanaofundisha serikalini na shule za binafsi ni walewale na wamesoma vyuo vilevile, lakini wanapoenda shule binafsi wanafanya vizuri. Kwa nini wasifanye vizuri hata wanapokuwa katika shule za serikali’? Amesema Akwilapo.
Aidha, Dkt. Akwilapo amekemea tabia ya baadhi ya walimu kufanya kazi binafsi nyakati za masomo wakiwemo wale wanaoendesha pikipiki maarufu kama Bodaboda. Amesema hiyo ni moja ya sababu zinazokwamisha maendeleo ya elimu hapa nchini. Amewataka Wadhibiti ubora wa shule waboreshe njia za kufanya tathimini. Badala ya kuanza kutoa taarifa kwa walimu kabla ya kwenda kuwakagua, wawe na utaratibu wa kuvamia ili kuwabaini walimu wanaotoka kwenye vituo vyao vya kazi kabla ya wakati. Hilo litasaidia kuwafanya walimu wawe tayari muda wote.
Pia wadhibiti ubora wawe na kumbukumbu ya watu waliokwisha wakagua badala ya kujikuta wanamkagua mwalimu mmoja tu kila wanapotembelea shule husika.
Kwa upande wake Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Kathleen Sekwao amemtaka Katibu Mkuu kuhakikisha mkoa wa Mtwara na hasa wilaya ya Nanyumbu inaangaliwa kwa jicho la pekee ili kutatua changamoto nyingi zilizopo. Amesema wao kwa upande wao watahakikisha wanautangaza mkoa kwa wadau mbalimbali ili wasaidiane na wenyeji katika kuinua kiwango cha elimu.
Pia ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kutatua changamoto mbalimbali za elimu kama vile kuongeza bajeti kulinganna na mahitaji yakiwemo mahitaji ya watoto wenye mahitaji maalumu. Na kutoa motisha kwa walimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.