Historia imeandikwa leo tarehe 28 Oktoba, 2024 baada ya kijiji cha Makome A, kilichopo ya kata ya Mbawala, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kuwashwa umeme hivyo kufanya jumla ya vijiji vyote 785 vya Mkoa wa Mtwara kuwa na umeme.
Akizungumza mara baada ya kuwasha umeme huo Mhe. Kanali Patrick Sawala, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara amepongeza wakala wa nishati vijijini (REA) kupitia Wizara ya Nishati kwa kufikisha umeme kwenye vijiji kwa 100% ambapo sasa kazi inaendelea kuunganisha umeme kwenye vitongoji.
“Mhe. Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mtwara una vijiji 785 na vyote sasa vina umeme kwahiyo upande wa vijiji hatuna deni. Ilani ya CCM ilitutaka tupeleke umeme kwenye vijiji vyote ifikapo 2025 tumekamilisha kabla ya hapo, ni jambo la kujivunia kimkoa.” Alieleza Bw. Jonas Olutu, Kaimu Mkurugenzi wa REA.
Mwenyekiti wa bodi ya REA, Balozi Meja Jenerali mstaafu, Jacob Kingu ametoa rai kwa wananchi hao kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000/= tu.
Katika hatua nyingine, Bw. Olutu alimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa Katika kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha itakayosaidia wananchi wa vijiji vya Tanzania bara kuweza kununua mitungi ya gesi kwa nusu bei, ambapo mkoa wa Mtwara mitungi ya gesi 16,275 itauzwa kwa nusu bei.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.