Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Mtwara leo Mei 18, 2025 zimeingia katika siku yake ya pili ambapo Mwenge umetembelea, umekagua, umeweka mawe ya msingi na kuzindua miradi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 3.5 katika Halmashauri ya Mji Masasi.
Mapema asubuhi Mwenge wa Uhuru uliweka jiwe la msingi katika Mradi wa Ujenzi wa barabara ya Nyasa shuleni yenye urefu wa kilometa 1 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 456 na baadae kuona na kukagua shughuli za vijana wa kikundi cha Jitihada Nyasa Chini.
Halikadhalika Mwenge wa Uhuru umezindua Mradi wa Ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya msingi Mkuti wenye thamani ya Shilingi milioni 83.4 na baadae Mwenge ulizindua nyumba ya watumishi wa afya katika kituo cha Afya Mtandi wenye thamani ya Shilingi milioni 95.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi hiyo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ndugu Ismail Ali Ussi amesema ameridhishwa namna miradi hiyo ilivyotekelezwa Kwa kiwango.
" Ndugu wanamasasi nichukue fursa hii kuwapongeza Kwa hatua hii nzuri ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo, nimejionea miradi yenu ya barabara, Ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja nyumba za watumishi wa afya kwa ujumla miradi imekidhi ubora wa viwango hongereni Sana" aliongeza Ndugu Ismail Ali Ussi.
Aidha Ndugu Ismail Ali Ussi pia ameiagiza Halmashauri ya Mji wa Masasi kuangalia uwezekano wa kupanua wigo wa kutoa mikopo Kwa utaratibu wa asilimia kumi yenye riba nafuu kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi.
Kuhusu umuhimu wa wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura Kiongozi wa Mbio za Mwenge Ismail Ali Ussi amewataka viongozi kuwahamasisha wananchi wenye sifa kuhakiki taarifa zao na wale ambao hawajajiandikisha kujiandikisha Ili waweze kupata haki ya kuwachagua viongozi wao katika uchaguzi mkuu ujao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.