Mkuu wa wilaya Mhe. Dunstan Kyobya amewaasa wahitimu wa kozi ya mafunzo ya jeshi la akiba kuutunza ujuzi waliopata kudumisha amani na kutetea maslahi ya Taifa.
Mhe. Kyobya ametoa wito huo katika hafla ya kufunga mafunzo ya jeshi la akiba iliyofanyika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na kusema kuwa serikali ina matumaini makubwa kuwa wahitumi hao watakuwa mfano wa kuigwa katika jamii.
"Ndugu wahitimu wa kozi hii ya jeshi la akiba, leo ni siku yenu muhimu inayoingia katika kitabu cha historia ya maisha yenu" alisema Kyobya.
"Nimeambiwa awali wakati mnaanza kozi hii mlikuwa 212, lakini kwa bahati nzuri 14 wakachaguliwa kujiunga na jeshi la kujenga Taifa, bila shaka hii ni faraja kubwa kwetu, sasa na nyinyi hakikisheni mnazingatia miiko na maadili mliyofundishwa na wakufunzi wenu itawasaidia kuaminika" alisema Mhe. Kyobya.
Halikadhalika Kyobya amesisitiza kuwa serikali inatarajia kuwa wahitimu hao watakuwa mabalozi wazuri wa mafunzo hayo na kujijengea imani na heshima katika jamii huku akiwataka kuweka mbele suala la uzalendo, uadilifu na nidhamu.
Pia Mhe. Dunstan Kyobya amelitumia jukwaa la hafla hiyo kuwahakikishia wahitimu kuwa, serikali inatambua changamoto ya ajira inayowakabili na kusema kuwa tayari Uongozi wa Wilaya na Mkoa unafanya jitihada za kuwasiliana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi zenye mahitaji ya vijana wenye sifa za mafunzo ya aina hiyo ili watoe kipaumbele katika ajira pindi zitakapojitokeza.
Jumla ya wahitimu 198 wametunukiwa vyeti vya kozi ya mafunzo ya miezi 6 ya Jeshi la akiba yaliyoanza mwezi Julai Mwaka huu ambapo kati ya hao 144 ni wanaume na 54 ni wanawake.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.