Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Halima Dendego kitabu cha Mpango Kabambe wa Mji wa Mtwara katika Hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Boma Mkoa jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi amezindua Mpango Kabambe wa Mji wa Mtwara huku akiutaka uongozi wa Mkoa wa Mtwara kutumia fursa hiyo kutangaza mkoa ili kuvutia wawekezaji.
Mpango huu ambao umekamilika kwa ushirikiano wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo na Makazi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara pamoja na Halmashauri za Manispaa ya Mtwara Mikindani na ile ya Wilaya ya Mtwara unashirikisha eneo lote la Manispaa ya Mtwara Mikindani na Kata 9 za Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Akiwahutubia waalikwa katika uzinduzi huo uliofanyika ukumbi wa Boma Mkoa ulioko Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara jana, Lukuvi amesema kwa muda mrefu mkoa ulisimamisha taratibu za kuendeleza mji huo ili kusubiri Mpango Kambambe ambao sasa umekamilika, hivyo fursa iko wazi kwa dunia nzima kuja kuwekeza Mtwara.
‘Ni suala jema kwa jinsi mlivyoamua kusimamisha uendelezaji wa ardhi ya ndani ya eneo hadi mpango huu ukamilike. Nashukuru mmesimamia vizuri na sasa wawekezaji wanakaribishwa kwa wingi.’ Alisema Lukuvi.
Mheshimiwa Lukuvi ambaye ameongoza Wizara hiyo kwa awamu mbili mfululizo amemshukuru Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda kwa Kusimamia vema mpango huo hadi kukamilika. Amesema Luanda ametumia vema taaluma yake ya Mipango Miji kuhakikisha mpango unakamilika katika hali nzuri, hivyo ni jambo la kupongeza.
Kuhusu taratibu ndani ya eneo la Mpango kabambe Mheshimiwa Lukuvi amewataka wananchi waondowe hofu ya kupoteza ardhi zao kwani mpango hauji kunyang’anya ardhi bali kuongeza thamani. Kwa wale watakao lazimika kupisha maeneo kwa ajili ya kuruhusu aina ya ujenzi uliopendekezwa katika mpango, watalipwa fidia katika thamani ya ardhi yao. Aidha mamlaka ya kiutawala pia hayabadilika.
Kuhusu faida za Mpango Kabambe, Lukuvi amesema mpango utasaidia kukabiliana na ongezeko la watu na utachochea watu kuja kuwekeza Mtwara na kuharakisha upangaji na upimaji wa rdhi. pia utapunguza migogoro ya ardhi hatimaye kuifikisha Mtwara katika uchumi wa viwanda
Aidha Mheshimiwa Lukuvi amewaonya wananchi wanaoendelea na ujenzi holela kuwa wasitarajie kubadili matumizi ya ardhi katika eneo ambalo watakuwa wamejenga bila utaratibu, badala yake watachukuliwa hatua za kisheria. Amewataka wananchi wote kuhakikisha wanafuatilia kwa viongozi wa halmashauri husika ili kujua mipango iliyoko katika eneo husika kabla ya kununua.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Halima Dendego amemshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kukubali kuzindua Mpango huo.
Amesema Mtwara imekuwa katika kasi ya kufunguka katika mambo mengi ikiwemo miradi mingi inayokuja ambayo ni pamoja na mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kilometa 1000 kutoka mchuchuma, barabara zinazojengwa na kupanuliwa na upanunzi wa uwanja wa ndege. Pia Uchumi wa korosho ambapo mkoa unazalisha zaidi ya asilimia 70 ya korosho yote hapa nchini. Amesema haya yote yataufanya mji kukua kwa haraka zaidi.
Akizungumzia hatua iliyofikiwa katika kuandaa mpango huu. Afisa Mipango Miji Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani Hamza Sikamkono amesema Matumizi ya makazi, viwanda na ongezeko la watu ni moja ya mambo yaliyowasukuma kukubaliana na wenzao wa halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kuandaa mpango huo.
Aidha, wanaamini kuwa mpango huo utasaidia kudhibiti ukuaji wa mji na ujenzi holela. Pia utawezesha kupanga maeneo mbalimbali ya mji, kuboresha na kuwezesha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.
Ameyataja maeneo yaliyoko katika mpango kuwa ni;
Eneo mahususi la Kisasa la Mjini Kati: Kitovu cha shughuli za kisasa za biashara, huduma za kibenki, Makao Makuu ya Taasisi Mbalimbali, Hoteli, majengo marefu na ya kisasa.
Eneo Mahususi la Naumbu: Kitovu cha ajira kwa wakazi wa mji hasa zitokanazo na shughuli za viwanda vikubwa Hekta 10-20, Makazi yaliyopangika na kuratibiwa kwa ustadi na maeneo ya mahoteli ya kitalii.
Eneo Mahususi la Mjimwema: Kitovu cha huduma za elimu ya juu hasa vyuo vikuu na makazi yaliyopangwa na kuratibiwa kwa ustadi wa hali ya juu.
Eneo mahususi la Nanguruwe: Kitovu cha huduma za kisasa za Afya, Viwanda vya ukubwa wa kati ya Hekta 5-9, Eneo la makazi ya kisasa yaliyopangwa na kuratibiwa kwa ustadi pembezoni ya mji, maeneo ya kilimo cha mjini kwa ajili ya ajira za wakazi wa Mtwara na kituo cha kisasa cha michezo.
Eneo mahususi la Ziwani: Kitovu cha huduma za Usafiri na Usafirishaji ambapo kuna eneo la kutosha la uwanja wa ndege wa kisasa, kituo kikubwa cha mabasi, garimoshi la abiria na mizigo, kituo cha biashara, n.k
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.