MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MKOANI MTWARA.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Kenan Sawala Aungana na wananchi Wilayani Masasi katika Kijiji cha Nagaga kwa ajili ya Maadhimisho hayo ya Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sherehe hizo zimepambwa na Matukio mbali mbali ikiwemo Uvutaji wa Kamba ambapo timu ya RS Mtwara ilishinda mchezo huo, Kukimbiza kuku na vikundi vya ngoma na nyimbo mbali mbali.
Katika sherehe hizo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Kenan Sawala akapata nafasi ya kuzungumza na wananchi ambapo alianza kwa kusema, napenda kutoa shukran zangu za kipekee kwa uongozi wa Wilaya ya Masasi na Wilaya nyingine pamoja na kamati za maandalizi katika ngazi ya Mkoa, Wilaya katika kazi kubwa ya kuhakikisha sherehe hizi zinafanyika kwa kufana. Nawashukuru wote kwa ushirikiano wenu ambao ni msingi wa mafanikio ya sherehe hizi, Hongereni sana.
Aidha, sherehe za mwaka huu ni maalum na za kipekee kwa kuwa Tanzania inatimiza miaka 60 ya Muungano. Hivyo tuna kila sababu ya kujivunia kwa kudumisha mahusiano ya kidugu na kijiografia kwa wananchi wa pande zote za Muungano.
Wote kwa pamoja turejee msisitizo wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipohutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Aprili 2021, alisisitiza kuijenga nchi yetu kwa kuzingatia Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na kujenga upya nchi.
Kanali Sawala akaendelea kwa kusema Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa Mikoa iliyofaidika na matunda ya Muungano huo. Katika miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumeshuhudia mafanikio makubwa ya kujivunia ikiwemo kuimarika kwa amani na utulivu ndani ya Mkoa wetu.
Aidha, tumeshuhudia namna serikali inavyoendeshwa kwa uwazi chini ya misingi ya sheria, Demokrasia na Utawala bora.
Pia kanali Sawala akazungumzia juu ya miradi iliyotekelezwa na miradi inayoendelea kutekelezwa ikiwemo Upanuzi wa Bandari ya Mtwara, Upanuzi na Ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Mtwra, Kuanza kwa ujenzi wa Barabara ya Uchumi Mtwara – Tandahimba – Newala – Masasi km 210, Ujenzi wa Hospitali ya rufaa ya kanda ya Kusini, Mapokezi ya shilingi Bil. 8 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vipya 12 vya kutolea huduma za dharura za uzazi na ununuzi wa vifaa tiba kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya katika ngazi ya Msingi.
Halikadhalika Kanali Sawala akatumia nafasi hiyo kuwakumbusha Wananchi juu ya yafuatayo, Kushiriki kutoa maoni ya Dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2050, Kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotegemewa kufanyika kuanzia mwezi oktoba, Kuongeza kasi ya matumizi ya nishati mbadala kwa ajili ya utunzaji wa mazingira yetu na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na Mkoa kwa ujumla.
Aprili 26, 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.