Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mtwara anayeshughulikia Rasilimali Watu, Renatus Mongogwela amekabidhi pikipiki 12 kwa Maafisa Tarafa wa Tarafa 12 Mkoani Mtwara.
Pikipiki hizo zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Aprili 6. 2019, baada ya kufanya kikao-kazi na maafisa Tarafa wote nchini alipokutana nao Ikulu jijini Dar es Salaam.
Hii inafanya Maafisa Tarafa wa Tarafa zote 31 za mkoa wa Mtwara kuwa na usafiri wa Pikipiki ambapo June 20, 2018 Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa aliwakabidhi Maafisa Tarafa 20 pikipiki zenye thamani ya shilingi milioni 48. Fedha hizo zilipatikana baada ya Serikali ya Mkoa kuzitenga kutoka bajeti yake ya mwaka 2017/2018.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mongogwela amewataka maafisa Tarafa hao kuhakikisha wanazitunza pikipiki hizo. Amesema serikali ina nia ya dhati kuhakikisha inatatua changamoto zinazowakumbwa watumishi wote wa umma hivyo wasikate tamaa pale wanapokutana na changamoto.
Naye Dotto Omari Nyirenda, Afisa Tarafa Tarafa ya Mchichira wilayani Tandahimba amemshukuu Mheshimiwa Rais kwa msaada huo na kwamba Pikipiki hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya usafiri. Amesema walikuwa wakilazimika kukodi usafiri na hivyo kutumia gharama kubwa kuendesha Tarafa. “Tunaenda kuchapa kazi kwani changamoto kubwa iliyokuwa ikitusumbua kwa muda mrefu imepatiwa ufumbuzi”. Amesema Dotto.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.