Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele kuanzisha mashamba darasa ya ufuta mkoani hapa.
Agizo hilo amelitoa leo Juni 12, 2019 wakati akizindua mafunzo ya matumizi sahihi ya viuatilifu kwa wakulima na Maafisa Ugani katika kijiji cha Maili Kumi wilayani Mtwara. Amesema mashamba hayo yatasaidia kutoa elimu kwa wakulima wa ufuta na hivyo kuongeza uzalishaji wa zao hilo. Pia, itapanua uelewa wa teknolojia ya kilimo na kuachana na imani ya baadhi ya wakulima kuwa shamba la ufuta linahitaji kupumzishwa kila baada ya msimu mmoja wa kilimo.
Amezitaja baadhi ya wilaya ambazo zinaweza kuanzishwa mashamba hayo ambayo yatamilikiwa na Halmashauri kuwa ni Masasi, Nanyumbu na Mtwara.
“Dkt. Kapinga, Tunahitaji kuwa na shamba la mfano. Wasiliana na halmashauri ya Masasi tupate shamba kubwa la halmashauri ambalo tutalisimiamia kuonesha kilimo cha ufuta, Pia Nanyumbu na Mtwara.” Amesema Byakanwa.
Amesema ardhi ya kilimo cha ufuta ipo ya kutosha hivyo ni suala la wakulima kuwezeshwa elimu. Amesema kwa sasa mkoa umedhamiria kuendeleza kilimo hicho ambacho kimeingizwa katika mfumo wa stakabadhi ghalani kama ilivyo kwa zao la korosho.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendelea (TARI–Naliendele) Dkt. Fortunatus Kapinga amesema Taasisi iko tayari kutekeleza agizo hilo. Amesema kilimo cha mazao mbadala imekuwa ni moja ya maekezo yao kwa wakulima wanakapoanzisha mashamba mapya ya korosho hivyo ni suala la kuweka msisitizo na kuongeza elimu zaidi.
Mkoa wa Mtwara ni moja ya wazalishaji wakuu wa zao la korosho ambalo limekuwa likiuzwa kupitia utaratibu wa stakabadhi ghalani. Msimu wa 2019/2020 zao la ufuta pia limeingizwa katika utaratibu huo jambo ambalo linawafanya viongozi wa mkoa kuhakikisha wanasisitiza wakulima kuchangamkia zao hilo.
video yake hii HAPA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.