Mwenge wa Uhuru leo Juni 03, 2024 umeanza mbio zake Wilayani Newala ambako umezindua Miradi, umeweka mawe ya msingi pamoja na kutembelea, kukagua na kuona miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Mji wa Newala.
Ukiwa Katika Halmashauri hiyo Mwenge wa Uhuru umetembelea miradi 7 yenye thamani ya. Shilingi bilioni 4.25.
Mradi wa kwanza kutembelewa ulikuwa ni mradi wa ujenzi wa barabara ya makondeko hadi Mkunya kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 2 katika kijiji Cha Makondeko iliyogharimu kiasi Cha shilingi Milioni 949.9.
Akiweka jiwe la msingi katika mradi huo kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Ndg. Godfrey Mzava amemwagiza Wakala wa Barabara Vijijini TARURA kuhakikisha wanaweka mipaka inayotambulika kisheria kati ya barabara na makazi ya watu Ili kuepuka migogoro na wananchi.
Kisha Mwenge wa Uhuru ukaelekea katika shule ya sekondari ya Tulindane katika kijiji cha Lingana ambako umezindua shule hiyo.
Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Ndg. Godfrey Mzava amesema ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kuongeza kuwa utakuwa mkombozi kwa wakazi wa Kijiji hicho.
Kituo kilichofuata baada ya uzinduzi huo ni kituo Cha Afya cha Zulu katika kijiji Cha Lichungu ambapo Mwenge wa Uhuru pia ulizindua mradi huo unaomilikiwa na mtu binafsi Ndg. Issa Lalikila.
Mhe. Mzava amempongeza mmiliki wa kituo hicho kwa ubunifu wake wa kuwekeza katika sekta ya Afya hatua ambayo amesema itasaidia kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za Afya katika Mji wa Newala.
Ukiwa katika kijiji hicho cha Lichungu Mwenge wa Uhuru umetembelea kuona na kukagua shughuli za wajasiliamali, vijana, Wanawake na wenye ulemavu pamoja na kukabidhi madawati, viti na meza kwa shule za msingi na sekondari mradi wenye thamani ya shilingi Milioni 57.4.
Pia Mwenge wa Uhuru ulikagua na kuona mradi wa ujenzi wa Tanki la Maji lenye ujazo wa lita Milioni 6 katika kijiji cha Nambunga wenye thamani ya shilingi Bilioni 2.2.
Aidha kiongozi wa mbio za Mwenge Mhe. Godfrey Mzava alihitimisha ziara ya mbio za Mwenge katika Halmashauri ya mji wa Newala kwa kuona na kukagua shughuli za Malaria, UKIMWI, na Lishe. Pia alikagua klabu ya kupambana na dawa za kulevya, rushes pamoja na banda la kutoa elimu ya uchaguzi.
Mwenge wa Uhuru utaendelea kukimbizwa Wilayani Newala hapo kesho ambapo itakuwa zamu ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Juni 03, 2024
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.