Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 Mkoani Mtwara leo Juni 2 zimebisha hodi katika Wilaya ya Tandahimba.
Ukiwa Wilayani hapa Mwenge wa Uhuru umezindua Miradi, umeweka mawe ya msingi pia umetembelea na kuona Miradi 7 yenye thamani ya shilingi Bilioni 3.78.
Mara baada ya kuwasili Mwenge wa Uhuru ulielekea katika Kijiji cha Lembela Kata ya Mihambwe ambako ulikagua na kuona Miradi wa ufugaji kuku wenye thamani ya shilingi Milioni 33 unaolenga kuwawezesha vijana Kiuchumi.
Kisha Mwenge ulielekea katika Kata ya Kitama Kijiji Cha Kitama shuleni ambako uliweka jiwe la msingi katika Mradi wa Ujenzi wa Kituo Cha Afya Kitama Uliogharimu shilingi Milioni 469.
Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Ndg. Godfrey Mzava amewaambia mamia ya Wananchi waliojitokeza kuulaki Mwenge kuwa. Serikali imedhamiria kuwasogezea wananchii huduma za Afya huku akiitaka Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba kukikamilisha kituo hicho Ili kiweze kuwahudumia wananchi.
Kituo kilichofuata kulikuwa ni Tandahimba mjini ambako Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi Mradi wa Ujenzi wa barabara kiwango Cha lami wenye thamani ya shilingi Milioni 949.4.
Akizungumza katika eneo la Mradi huo Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Ndg. Godfrey Mzava amesema Serikali inatumika fedha nyingi kukamilisha miradi ya barabara huku akiwataka wananchi kuitunza ili idumu kwa muda mrefu.
Aidha Mzava amepongeza wakala wa barabara vijijini TARURA kwa kukidhi vigezo vya taratibu za manunuzi katika matumizi ya mfumo wa NEST.
Mradi mwingine uliotembelewa na Mwenge wa Uhuru mjini Tandahimba ni Mradi wa jengo la Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Mradi Uliogharimu kiasi Cha shilingi milioni 281.
Kisha Mwenge wa Uhuru ukaelekea Kijiji Cha Malamba Kata ya Malopokelo kukagua na kuona shughuli za upandaji miti na uhifadhi wa mazingira katika shamba la miti Malamba, Mradi uliogharimu shilingi Milioni 7.4.
Baadae ziara ya Mwenge wa Uhuru iliendelea katika Kata ya Mkundi katika Kijiji Cha Chitoholi A ambako Mwenge wa Uhuru uliweka jiwe la msingi katika mradi wa maji Chitoholi uliogharimu shilingi Bilioni 1.4.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa Ndg. Geoffrey Mzava amewaambia Wananchi waliofika kuulaki Mwenge kuwa Serikali kwa kutambua adha ya upatikanaji wa maji safi imeamua kuwekeza katika mradi huo na kuwataka wakazi wa Chitoholi na maeneo jirani kutunza miundombinu yake.
Aidha amewapongeza Wakala wa Usambazaji Maji Safi Vijijini na Usafi wa Mazingira RUWASA kwa kutumia vigezo vya mfumo wa manunuzi wa NEST ambao umeisaidia Serikali kuepuka hasara na vitendo vya ubadhilifu.
Mradi wa mwisho uliohitimisha ziara ya Mwenge wa Uhuru ni ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Makondeni mradi uliogharimu shilingi Milioni 560.5.
Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Mtwara 2024 zitaendelea tena hapo kesho Wilayani Newala.
Juni 02, 2024
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.