Wiki hii Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa amefanya ziara katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero zinazohusiana na masuala ya ardhi. Ziara hiyo ya siku mbili ilianza tarehe 27 na kukamilika tarehe 28.
Moja ya mgogoro aliousikiliza ni kuhusu mpaka kati ya makazi ya wananchi na eneo la uwanja wa ndege.
Akielezea kuhusu uhalali wa umiliki wa eneo lenye mgogoro Meneja uwanja wa Ndege Mtwara Emily Simbachawene amesema upimaji wa uwanja wa ndege Mtwara ulifanyika mwaka 1988 ambapo eneo lililobainishwa kuwa chini ya uwanja wa ndege ni hekta 1030 likiwemo eneo lenye mgogoro.
Mgogoro ulianza mwaka 2010 baada ya Menejimenti ya uwanja wa Ndege kupata taarifa za uvamizi wa mipaka ya uwanja. Menejimenti ilichukua uamuzi wa kuwaandikia wenyeviti wa mitaa inayozunguka eneo la uwanja pamoja na serikali ya Wilaya. Aidha baadaye ulifanyika utaratibu wa kupima eneo hilo lakini utekelezaji wake uliishia asilimia 50 baada ya kuzuiwa na wakazi wa Mangamba ambao walitishia kuwajeruhi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa wananchi wanaodaiwa kuvamia eneo, Valerian Tesha ameeleza kuwa baada ya kubainika kuwepo mgogoro, wananchi waliamua kuwasiliana na serikali ili kuondoa tatizo hilo. Juni 9, 2015 walimwandikia Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi ambapo tarehe 5/10/2015 barua ilijibiwa kwa kuwaandikia barua Manispaa kupitia Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kusini. katika barua hiyo Waziri alitoa siku 14 Manispaa wabainishe mipaka ya eneo la uwanja wa ndege, waoneshe ni wananchi wangapi walikutwa katika eneo wakati wa upimaji, ushirikishwaji wa wananchi wakati ardhi inachukuliwa, iwapo fidia ya ardhi ilitolewa, pia kama kuna maendelezo ya ardhi yaliyofanyika baada ya fidia. Alidai kuwa kutotekelezwa kwa maagizo yote hayo ndiyo kiini cha mgogoro huo.
Baada ya kusikiliza pande zote Mheshimiwa Byakanwa ameunda Kamati Maalumu iambayo ameiagiza kupitia nyaraka zote za migogoro hiyo na kumshauri nini kifanyike.
Bonyeza HAPA kupata picha na matukio yote yaliyojiri katika ziara hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.