Mgeni rasmi katika maadhimisho ya maiaka 63 ya Uhuru Tanzania bara mkoa wa Mtwara Mkuu wa wilaya ya Newala, Mhe. Rajabu Kundya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara leo tarehe 9 Disemba 2024 ametoa rai kwa Viongozi wa serikali za mitaa kushirikisha wananchi ili kuleta maendeleo katika maeneo yao.
“Mafanikio yaliyopatikana kisiasa, kiuchumi, kiulinzi, kijamii na kiteknolojia ni matunda ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya viongozi mbalimbali na wananchi mkoani Mtwara.” Alieleza Mhe. Kundya
Mhe. Kundya aliongeza kwa kusema; “Ninawasihi viongozi wote walioshinda katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa kuwashirikisha wananchi wote bila kujali vyama vyao vya siasa, itikadi za siasa na dini; wawashirikishe kikamilifu. Ushirikishwaji wa wananchi ndio msingi wa maendeleo yetu.”
Aidha, Mhe. Kundya amewasihi wananchi kuongeza jitihada ya kusimamia elimu ya watoto wa kike ili wawe sehemu ya mafanikio katika shule ya kisasa inayojengwa mkoani Mtwara, “Mradi wa ujenzi wa shule ya wasichana ya kitaifa kupitia fedha za SEIQUIP kwa thamani ya Bilioni 4 zimekwishapokelewa na mradi unaendelea.”
Akieleza mafanikio ya mkoa wa Mtwara yatokanayo na Uhuru, Mhe. Kundya alisema, Mkoa umepiga hatua kubwa za maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo usafiri ambapo korosho ya mikoa ya kusini inasafirishwa kupitia bandari ya Mtwara, kwa msimu huu wa kotosho mpaka leo jumla ya tani 125,169 zimesafirishwa na tani 30 elfu zimepakiwa tayari kusafirishwa.
“Mkoa umetumia jumla ya Bilioni 170 kwaajili ya uwekezaji wa umeme vijijini (REA) ambazo zimewezesha kuwasha vijiji vyote 785 vya mkoa wa Mtwara; mpango wa serikali kwa sasa ni kuanza mradi mwingine kuhakikisha vitongoji vyote vinapata umeme usio na mashaka ili kuchochea maendeleo katika mkoa wetu.” Alieleza Mhe. Kundya
Kauli mbiu ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania 2024; “UONGOZI MADHUBUTI NA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI NI MSINGI WA MAENDELEO YETU”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.