TAKWIMU za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zilizotolewa Februari, mwaka huu, zinaonyesha namna zao la korosho lilivyoliingizia taifa pato la dola milioni 346.6.
Pato hilo ni sawa na takriban sh. bilioni 773, ikilinganishwa na mwaka jana, ambapo nchi ilipata dola milioni 184.9, sawa na zaidi ya sh. bilioni 411.
Upatikanaji wa fedha hizo umewezesha korosho kuwa zao namba moja kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni nchini.
Mafanikio hayo ni mkakati wa serikali katika kushughulika na wote watakaojihusisha kuminya haki na manufaa ya mkulima mmoja mmoja, kikundi au ushirika.
Katika kufanikisha hilo, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika ameanza kuchukua hatua dhidi ya ubadhirifu wa fedha na mali za vyama hivyo nchini, baada ya kuvunja bodi 10 za vyama hivyo vya wakulima wa korosho.
Hatua hiyo inatokana na uchunguzi uliofanywa na serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC) kwa kushirikiana na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO).
Uchunguzi huo uliofanyika mwaka jana, ulibaini ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi na mali katika vyama hivyo kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara na hivyo kuamua kuitisha mikutano maalumu ya vyama hivyo kwa hatua zaidi.
Ifahamike kuwa, mwelekeo wa serikali kwenye sekta ya kilimo ni kuhakikisha inakuwa sehemu muhimu ya kuimarisha uchumi, kuongeza kipato cha mkulima na kuchochea ukuaji wa viwanda ili kuongeza ajira.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Mjaliwa, katika hotuba yake kwenye kikao kilichowakutanisha wadau wa zao hilo mapema mwaka huu, anasema korosho huendesha maisha ya kaya zaidi ya 500,000 kama zao kuu la kibiashara katika wilaya zaidi ya 30 kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga.
Na sasa idadi ya watakaokuwa wakiguswa moja kwa moja na korosho, inatarajiwa kuongezeka zaidi na pengine kufikia nusu ya Watanzania wote kutokana na mipango ya kupanua kilimo cha korosho.
Februali, mwaka huu, Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), ilianza mpango wa kugawa bure miche ya mikorosho kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Jumla ya miche milioni 10 inatarajiwa kusambazwa mwaka huu,
kwa wakulima wa mikoa mitano inayolima zao hilo ya Lindi, Pwani, Tanga, Mtwara na Ruvuma.
Tanzania inasimama katika nafasi nzuri ya kuongeza uzalishaji wa korosho ambalo kwa sasa ndilo zao pekee lililobaki lenye mipango endelevu na lenye soko lisiloyumba.
Serikali imefuta tozo tano kati ya tisa alizokuwa anakatwa mkulima baada ya kubainika kwamba, hazikuwa sahihi. Uamuzi huo umekuja baada ya malalamiko ya wakulima wa korosho ambao walikuwa wanatozwa tozo nyingi, hali iliyosababisha wauchukie mfumo wa stakabadhi ghalani.
Tozo hizo ni makato ya sh. 50 yaliyokuwa yanatozwa kwa kilo moja kwa ajili ya usafirishaji wa korosho kupeleka kwenye minada, asilimia moja inayokatwa kuiwezesha sekretarieti ya mkoa kusimamia zao hilo.
Tozo nyingine ni ya shilingi tano iliyokuwa inakatwa katika kila kilo moja kuchangia chama kikuu cha ushirika na gharama ya kulipia ghala, tozo ambazo hazikuwa na tija kwa mkulima.
Kutokana na jitihada hizo za serikali katika kuinua zao hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, anaeleza mikakati iliyopo ya kuboresha zaidi kilimo hicho mkoani humo.
Anasema mkoa ulifanya uhakiki wa tani 4,045 za salfa zilizopo katika maghala ya Mtwara inayosubiri kusafirishwa kwa wakulima ili kujiridhisha kama ina ubora wa kutumika.
Hatua hiyo itasaidia kuwawezesha wakulima kuepukana na uwepo wa salfa zisizokuwa na ubora, ambazo husababisha wakulima kupata hasara kutokana na mazao yao kuharibiwa na wadudu.
Mkuu huyo wa mkoa pia ameiagiza taasisi inayosimamia uingizaji wa viuatilifu kufanya tathmini ya ubora wa mzigo huo kabla haujaenda kwa wakulima.
“Wakulima wamekuwa wakipata matatizo hasa kutoka kwa baadhi ya wasambazaji wa viuatilifu wasiokuwa waaminifu, ambao wamekuwa wakisambaza viwatilifu ambavyo havina viwango vinavyotakiwa,” anaeleza.
Katika kufanikisha wakulima kuandaa mashamba yao mapema, mkoa huo umejizatiti kufanikisha pembejeo za korosho zinafika mapema ikilinganishwa na misimu iliyopita.
“Kutokana na hatua hiyo, uhamasishaji wa palizi na upuliziaji ulifanyika kwa mafanikio hivyo ilisaidia kupungua kwa malalamiko ya wakulima kuhusiana na ubora na utoshelevu wa pembejeo,” anafafanua.
Licha ya mafanikio na mikakati hiyo, bado kuna baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi.
Halima anaeleza changamoto hizo ni uwepo wa vituo vichache vya ugawaji pembejeo na upungufu wa pembejeo hali iliyosababisha msongamano mkubwa wa mawakala.
Zingine ni gharama kubwa ya usafirishaji wa fedha kwenda kwa wakulima na upungufu wa fedha katika benki, hivyo kutumia muda mrefu ukitumika kwa ajili ya kulipa fedha za wakulima.
“Lakini pia uaminifu mdogo kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi na vyama vikuu kushindwa kujiendesha kwa ushuru wa sh. 10 kwa kilo,” anaeleza.
Mkuu huyo anawataka wadau kufahamu kuwa, korosho ni dhahabu ya kijani, dhahabu yenye thamani kubwa, hivyo wapo watu wazuri wenye kuitakia mema na wabaya ambao wamekuwa wakiihujumu.
Anawataka wadau wa korosho kushikamana na kuwa wamoja ili kuleta mafanikio zaidi kwa wakulima wote wa zao hilo katika mkoa huo.
Kama anavyosema Halima, zao la korosho ni dhahabu, ni muhimu kwa kila mmoja kulithamini, kwa kuwa lina uwezo wa kumfanya mkulima kuishi maisha ya hali ya juu.
Hiyo inatokana na ukweli kwamba, kama ambavyo dhahabu inagombaniwa duniani, ndivyo ambavyo korosho inavyopiganiwa na wale wanaojua thamani yake.
Kitu muhimu ni kwa wadau na serikali kuzidisha elimu kwa wakulima juu ya aina bora ya kilimo cha zao hilo, ili liweze kuwanufaisha zaidi wakulima na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia.
Pamoja na elimu bora na njia bora za kilimo cha zao hilo, pembejeo nazo zinatakiwa kuwafikia wakulima kwa wakati badala ya kuzisubiri kwa muda mrefu, kitu ambacho kinawapa changamoto katika shughuli zao.
Pembejeo zinapaswa ziwe na kiwango bora, kutokana na kuwepo baadhi ya wafanyabiashara wanaochakachua na kuzipotezea ubora unaostahili, hivyo kuwapa wakulima hasara.
hivyo, kila mdau wa maendeleo anatakiwa kuendelea kuunga juhudi za serikali katika kuhakikisha korosho linakuwa zao adhimu la kibiashara ambalo litaingiza fedha nyingi za kigeni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.