Mkuu wa mkoa wa Mtwara kanali Patrick Sawala amewataka viongozi wa vyama vya msingi na wanachama wa vyama vya msingi mkoani Mtwara kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wabadilike na kufanya kazi kwa uadilifu ili kuleta tija kwa wakulima.
Kanali Sawala ametoa agizo hilo wakati anazungumza na viongozi hao kwenye jukwaa la ushirika lililokuwa na lengo la kujadili changamoto na mafanikio katika sekta ya ushirika mkoani humo.
Amesema wale viongozi wa ushirika wanaofanya ubadhirifu wa fedha za wakulima kwa makusudi ili kujinufaisha waache mara moja kufanya hivyo wakiendelea mkono wa sheria utawashughulikia.
Kanali Sawala amewasisitiza viongozi hao kuacha kuchukua fedha za wakulima ambapo tumeanza msimu wa ufuta kisha mbaazi zitafuata sitaki kusikia mkulima amedhulumiwa hela zake naaamini hata msimu wa korosho ukifika fanyeni vizuri sitaki kusikia malalamiko ya wakulima.
Mkuu huyo wa mkoa ametumia jukwaa hilo kuwataka viongozi hao kujipanga kuongeza uzalishaji katika mazao yote ikiwemo korosho, ufuta, mbaazi na sasa ni zao la choroko lakini pia wakumbusheni wakulima kulima mazao mchanganyiko yakiwemo mazao ya chakula na biashara ili kujiongezea kipato.
Halikadhalika Kanali Patrick Sawala amezitaka taasisi za kifedha mabenki kufanya taratibu zao kwa umakini ili waweze kulipa fedha za wakulima kwa wakati bila mkulima kupata usumbufu wa kucheleweshewa malipo yake.
Katika hatua nyingine amewasisitiza viongozi wa vyama vikuu vya ushirika ambao ndio wasimamizi wakuu wa ushirika kusimamia ipasavyo malipo ya wakulima katika msimu huu yaende vizuri na katika misimu yote inayokuja malipo yaende vizuri kwa wakulima sambamba na kuwataka waendesha maghala ambao sio waaminifu wamekuwa wakileta changamoto kwenye kuhifadhi mazao wasipewe nafasi ya kupewa maghala.
Akihitimisha hotuba yake kwenye jukwaa hilo la ushirika mkuu wa mkoa wa Mtwara kanali Patrick Sawala amewakumbusha viongozi kuhakikisha wanapiga kura kwenye uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba mwaka huu kwa amani na utulivu .
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.