Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa akipanda mti wakati wa uzinduzi wa upandaji miti Kimkoa Mtwara
Mkoa wa Mtwara umeazimia kupanda miti milioni sita katika kipindi cha mwaka 2018. Miti hiyo itapandwa kupitia makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo Halmashauri za Wilaya, watu binafsi, vikundi na Taasisi mbalimbali za Kiserikali na zisizo za Kiserikali. Aidha, aina ya Miti inayotarajiwa kupandwa ni pamoja na miti ya mbao, mijengo, kuni, mapambo, matunda na miti kilimo hususan mikorosho, michungwa na miembe.
Hayo yamesemwa wiki hii na Katibu Tawala Msaidizi uchumi na uzalishaji mkoa wa Mtwara Amani Rusake wakati wa uzinduzi wa kampeini ya upandaji miti kimkoa uliofanyika katika kijiji cha Muungano kilichoko kata ya Lulindi wilayani Masassi Mkoani Mtwara.
Amesema tangu miaka ya nyuma mkoa umekwa ukihamasisha upandaji miti ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu tangu 2015 mkoa umepanda miti 11,296,447. Mwaka 2015 mkoa ulipanda miti 3,250,442, Mwaka 2016 miti 3,353,273, Mwaka 2017 miti 4,692,732.
Ameitaja changanmoto ya ukataji miti hovyo kuwa ni moja ya sababu ya kupungua kwa misitu na kwamba mkoa umejipanga kupambana na hali hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa amesema ukataji wa miti kiholela haukubaliki hivyo amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanasimamia uzuiaji wa ukataji wa miti hovyo. Aidha ametoa wiki tatu kuhakikisha anapata taarifa ya orodha ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ukataji miti kwa ajili ya mkaa na vituo vya kukusanyia mkaa, orodha ya watengeneza mkaa, Ushahidi wa miti isiyopungua 1,000 au zaidi iliyopandwa wakati wa msimu wa mvua na kila mtengenezaji wa mkaa aliyepata leseni kutoka Wilayani.
Pia ameagiza sehemu ambapo hazipo Kamati za mazingira za vijiji zinazohusika pia na suala la upandaji miti zianzishwe mara moja. Vilevile Kila kijiji kiwe na shamba au mashamba maalum ya miti kwa ajili ya matumizi ya nishati (kuni, mkaa) na biashara ya mbao.
Sambamba na maagizo hayo Mheshimiwa Byakanwa ameagiza kila Mkuu wa Wilaya kuzindua kampeini hii wilayani kwake ili mkakati huu wa upandaji miti uwafikie na kueleweka kwa wananchi wote.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.