Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapteni Mstaafu Mhe. George Huruma Mkuchika amewataka wananchi wa Mtwara kuchangamukia Elimu.
Mheshimiwa Mkuchika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini ameyasema hayo akiwa katika kijiji cha Lwelu kilicho Manispaa ya Mtwara Mikindani ambako alikuwa akikagua miradi inayotekelezwa kupitia mpango wa TASAF.
Akitumia maandiko matakatifu Mheshimiwa Mkuchika amesema hata Kitabu cha Mithali ndani ya Biblia Takatifu kinawataka wakristo kuishika sana Elimu na wasiiache, halikadhalika Quran Takatifu inawataka waislam kuitafuta sana elimu hata kama ni kwa kuifuata nje ya Nchi.
Amesema yeye kama mzaliwa na Mtwara na Mbunge wa jimbo ndani ya Mkoa wa Mtwara haridhishwi na hali ya eilimu mkoani Mtwara. Amesema mkoa umekuwa ukishika nafasi za mwisho katika mitihani ya Taifa kutokana na wananchi wa mkoa wa Mtwara kutoweka jitihada kubwa katika elimu.
Amewataka wazazi kuhakikisha watoto wanafanya vizuri katika mitihani kwa kutimiza wajibu wao. Ametaja moja ya majukumu makubwa ya wazazi kuwa ni pamoja na kuchangia mambo mbalimbali ya kielimu ikiwemo kuwawezesha watoto kupata huduma ya chakula.
‘Nimekuja kufuatilia mambo ya TASAF lakini lazima niliseme hili kwani TASAF inatoa misaada mbalibmali ya kuwawezesha watoto kwenda shule lakini wazazi wana nafasi ya kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa katika mpango yanafikiwa huku na wao wakifanya jitihada zao binafsi kuhakikisha watoto wanapata elimu’. Alisema Mkuchika
Awali wakiwasilisha taarifa ya hali ya maendeleo ya utekelezaji wa Miradi ya TASAF wananchi wa kijiji hicho walielezea changamoto ya Elimu ambapo vipo vijiji ambavyo vinasafari umbali mrefu kuifuata elimu na hivyo kumtaka waziri asaidie kutatua changamoto hiyo.
Akifafanua suala hilo Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Evod Mmand amesema anatambua changamoto hiyo na kuahidi kuifanyia kazi.
Mkoa wa Mtwara Umekuwa haufanyi vizuri katika mitihani ya Kitaifa ambapo matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Pili 2017 mkoa ulitoa shule 9 za mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.