Mkuu wa Mkoa wa Mtwara mapema leo hii amefungua Kampeni Ya Kitaifa Ya Chanjo Ya Surua Rubella Tarehe 16 Februari, 2024 Katika Kituo Cha Afya Ufukoni – Manispaa Ya Mtwara Mikindani.
Ambapo amesema “napenda kuwashukuru ninyi nyote kwa kukusanyika kwenu mahali hapa, hii ni dalili nzuri na ishara kwamba mnajali afya za watoto wetu na Taifa kwa ujumla kwa kuwakinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo na hatimaye kupunguza vifo.”
Aidha Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na wadau imeandaa kampeni shirikishi ya kitaifa ya kutoa chanjo ya Surua Rubella kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano (Miezi 9-59) kuanzia tarehe 15 hadi 18 Februari, 2024.
Lengo mahususi la kampeni hii ni kuzuia na kupambana na ugonjwa wa Surua Rubella kwa kutoa chanjo kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka 5 kutokana na ukweli kwamba watoto wenye umri chini ya miaka 5 ndo huathirika zaidi unapotokea mlipuko.
Kanali Ahmed asema kupitia kampeni hii ndani ya Mkoa wetu, watoto wapatao 172,062 wataongezewa kinga kwa kuwapatia chanjo hata kama walishapata chanjo hizo kupitia utaratibu wa kawaida wa huduma za chanjo kupitia kliniki. Niwaombe wataalamu wetu kutoa chanjo hizi kwa walengwa wote kwa upendo na kwa umakini mkubwa sana ili lengo la kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa Surua na Rubella litimie. Wajibu wetu kama viongozi, wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla ni kuhamasishana na kuhakikisha tunajitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wetu kwenye vituo vya kutolea chanjo vilivyopangwa ili kuhakikisha kila mlengwa anafikiwa katika eneo husika, na tuwe mstari wa mbele kukanusha upotoshaji unaoweza kujitokeza dhidi ya kampeni hii au chanjo kwa ujumla wake.
Aidha nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri, Wataalamu wa Afya, Viongozi wa ngazi zote na wadau mbalimbali ndani ya Mkoa kuendeleza hamasa Sambamba na kuelimisha wananchi kwa kila kata, vijiji, vitongoji na Mitaa ili wajitokeze kwa wingi kuwaleta watoto wote wanaostahili kupatiwa chanjo hizi.
Kanali Ahmed akamalizia kwa kuwakumbusha kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya Mkoa. Tuwe wasimamizi na waangalizi namba moja wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Vituo vya kutolea huduma za Afya vimejengwa kwa wingi ndani ya Mkoa wetu ikiwemo kituo hiki cha Ufukoni. Hivyo ni wajibu wetu kuvitunza ili vunufaishe vizazi na vizazi katika utoaji wa huduma bora za Afya.
Februari 16, 2024.
#TunaifunguaMtwara
#KaziIendelee
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.