Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewataka watumishi katika ngazi mbalimbali kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi ili kupunguza kero zinazorudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kanali Ahmed ametoa kauli hiyo wakati wa makabidhiano ya ofisi katika ukumbi wa boma mkoani Mtwara leo ambapo amesema miongoni mwa mambo atakayohakikisha anayasimamia kikamilifu ni pamoja na suala zima la ukusanyaji mapato, ubunifu wa miradi pamoja na maboresho katika sekta ya elimu.
Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameongeza kuwa atahakikisha anaendeleza mambo yote mazuri yaliyoasisiwa na mkuu wa mkoa aliyemaliza muda wake Meja Jenerali Marco Gaguti na kuwataka watendaji wote kumpa ushirikiano ili aweze kutimiza ndoto za wanamtwara.
“Ndugu zangu nawaahidi utumishi uliotukuka, niko tayari kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo, nitashirikiana na nyinyi bega kwa bega naomba msisite kunifahamisha mikakati mizuri mliyokuwa mmeipanga ili tuiendeleze kwa pamoja” alisisitiza kanali Ahmed Abbas.
Halikadhalika Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewaagiza viongozi na watendaji katika ngazi zote kuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la sense ya watu na makazi Agosti, 23 ili serikali iweze kupata takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga mipango endelevu.
Aidha Kanali Ahmed amempongeza aliyekuwa mkuu wa mkoa wa mtwara Meja Jenerali Marco Gaguti na kusema kuwa wakati wote wa uongozi wake katika maeneo mbalimbali aliyopita amekuwa ni kiongozi wa mfano ambopo iliwalazimu baadhi ya viongozi wenzake akiwemo yeye mwenyewe kumtembelea kujifunza mbinu alizokuwa akitumia.
“ Meja Jenerali Marco Gaguti kwangu mimi ni mwalimu, nawathibitishia nimejifunza mengi kutoka kwake na nimekuwa nikifuatilia namna alivyokuwa akiuongoza mkoa huu, kwa ujumla sitakuwa na kazi kubwa zaidi ya kuendeleza maono yake, hongera sana mheshimiwa” aliongeza Kanali Ahmed Abbas.
Kwa upande wake aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mtwara Meja Jenerali Marco Gaguti amewashukuru wanamtwara kwa ushirikiano waliompa wakati wote wa uongozi wake na kusema kuwa walimsaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha kazi yake.
“ Mheshimiwa Mkuu wa mkoa naomba nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi wote wa mkoa wa Mtwara, watendaji pamoja na wananchi kwa ujumla, ninaamini ushirikiano walionipa wakati wote nilpokuwa hapa ndio umeniwezesha kufika hapa nilipo ninawashukuru sana” alisema Meja Jenerali Gaguti.
Halikadhalika Meja Jenerali Gaguti amewataka viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mtwara kumpa ushirikiano Mkuu wa Mkoa kanali Ahmed Abbas Ahmed ili aweze kuzisimamia kikamilifu ajenda muhimu za mkoa ikiwemo uchumi na elimu.
Meja Jenerali Marco Gaguti ameutumikia Mkoa wa Mtwara kwa zaidi ya mwaka mmoja ambapo wiki iliyopita Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alimpandisha cheo kutoka Brigedia Jenerali na kuwa Meja Jenerali.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara Yusuf Nnanila amesema chama kitampa ushirikiano wa kutosha na kuongeza kuwa uzoefu wake katika uongozi utamsaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Halikadhalika Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Abdallah Malela amemuahidi mkuu wa Mkoa kuwa ataendelea kuwasimamia kikamilifu watendaji kwa kasi ile ile ili kuhakikisha malengo ya Mkoa yanatimia.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed alikuwa mkuu wa wilaya ya Kibiti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.