Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya amewataka wananchi, wafanyabiashara, kampuni na taasisi kujitangaza kupitia tamasha la ufukweni la Msanga Mkuu (Msanga Mkuu Beach Festival) linalotarajiwa kufanyika katika kijiji cha Msanga Mkuu nje kidogo ya mji wa Mtwara kuitumia fursa hiyo huku akisisitiza kuwa maandalizi yote ya shughuli hiyo yanaendelea vizuri.
Mhe Kyobya ametoa kauli hiyo leo katika eneo la fukwe ya Msanga Mkuu wakati wa ziara yake ya kukagua hatua za maandalizi ya tamasha hilo ambapo amewaagiza wajumbe wa kamati maalumu kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote ikiwemo kusambaza huduma muhimu za kijamii kwa wakati.
“Ndugu zangu wanakamati bila shaka mmejionea hali halisi ya maandalizi ya eneo letu, ni matarajio yangu nikifika tena mahali hapa nitakuta miundombinu ya umeme, barabara, maji na maliwato vimekamilika, TANESCO, TARURA, MTUWASA pamoja na taasisi nyingine zote zinazohusika wajibikeni kulifanikisha hili” aliongeza Mhe. Kyobya.
Akiambata na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya amesema tamasha hilo litasaidia kuzitangaza fursa na vivutio mbalimbali vinavyopatikana mkoani Mtwara zikiwemo fukwe, maeneo ya uwekezaji pamoja na mila na desturi za wakazi wa kanda ya kusini.
“Mtwara ni mkoa ambao baadhi ya watu wamekuwa wakiusikia kupitia vyombo vya habari, lakini kupitia tamasha hili naamini watajionea wenyewe vivutio mbalimbali ikiwemo bandari yetu ya Mtwara inayoonekana hapo mbele yenu, si hivyo tu pia vyakula vya kiasili vitakuwepo katika eneo hili, halikadhalika michezo mbalimbali ya ufukweni, kwa kweli sidhani kama kuna mtu atakubali kupitwa” alisisitiza Mhe. Kyobya.
Aidha Mhe. Kyobya aliongeza kuwa katika jitihada za kuboresha mikakati ya maandalizi ya tamasha hilo kamati imekubaliana mnamo Disemba 18, siku ya fainali ya kombe la Dunia itakuwa ni siku maalum ya uzinduzi wa awali wa tamasha hilo, ambapo wananchi wote wataruhusiwa kushuhudia fainali hiyo mubashara kupitia runinga kubwa bila kiingilio.
“Ndugu zangu nachukua fursa hii kuwakaribisheni nyote siku hiyo ya fainali, tumejipanga na huduma zote muhimu za kijamii zitakuwepo, pia pokeeni salamu za Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed Mkuu wa mkoa wetu, anawatakia maandalizi mema ya shughuli hii, bila shaka tutakuwa naye katika tukio kuu la uzinduzi Disemba 24’’ aliongeza Mhe. Kyobya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi Athumani Kambi amemhakikishia Mkuu wa wilaya kuwa wajumbe wote wa kamati yake wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha shughuli hii inafanikiwa ambapo mpango kazi wa eneo lenye ukubwa wa takribani ekari 10 umekamilika na tayari miundombinu muhimu imeanza kuwekwa.
Jumla ya washiriki wapatao 20,000 wanatarajiwa kuhudhuria Tamasha la ufukweni la Msanga Mkuu ambalo ni la tatu tangu kuasisiwa kwake mnamo mwaka 2018.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.