Katika kuhakikisha Mtwara inazidi kufunguka kiutalii, Mhe. Mwanahamisi Munkunda, Mkuu wa wilaya ya Mtwara kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa jana tarehe 28/08/2024 amezindua rasmi Tamasha la Nyangumi 2024 rasmi katika viwanja vya Mashujaa.
“Mtwara una vivutio vingi vya kiutalii ambavyo bado havijulikani kwa watu, ni kiu ya Mhe. Rais Samia kuona mkoa wa Mtwara unafunguka kiutalii na kiuchumi; tayari tumeanza kutumia bandari ya Mtwara kusafirisha mazao ya korosho sasa tutangaze vivutio vyetu ikiwemo msimu huu wa Nyangumi ili wageni waje lakini pia na sisi wakazi twende tukafanye utalii wa ndani.” Alieleza Mhe. Munkunda
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo, Mhifadhi Mfawidhi wa Marine Park, Dkt. Reidfred Ngowo alisema Nyangumi huonekana katika Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingiliano ya Mto Ruvuma kuanzia mwezi Julai mpaka Novemba kila mwaka kwani mazingira ya hayo ni rafiki kwao kwa kukidhi mahitaji yao ya kujamiiana, kuzaana na kulea.
“Nyangumi wamekuwa kivutio kwa watu ndani na nje ya nchi kwa kuwa wana sifa za kipekee ikiwa ni pamoja na kuwa ni viumbe wakubwa wanaoishi majini wakiwa na uzito unakadiriwa kufikia tani 40. Pia nyangumi hubeba mimba kwa kipindi cha miezi 12 na mtoto wake huzaliwa akiwa na
uzito wa kilogramu 900 hadi 1000 huku akiwa na uwezo wa kuzaa kila baada ya miaka mitatu.” Alieleza Dkt. Ngowo
Tamasha hilo limelenga kujenga uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa rasilimali ambazo zinahifadhiwa na kutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo kujenga hoteli.
Kwa upande wake, Mhifadhi wa Bahari, Mussa Ally ameitaka jamii ya wavuvi kutowavua Nyangumi kwani husaidia kunyonya hewa ya ukaa ambayo inaleta athari kubwa.
Aidha, Maonesho hayo yanaendelea katika viwanja vya Mashujaa mpaka tarehe 06/09/2024 ambapo wananchi watapata fursa ya kujiandikisha kwaajili ya kwenda Msimbati maadhimisho ya kilele cha Tamasha la Nyangumi tarehe 07/09/2024
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.