Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed leo amefika katika Ofisi za GSM jijini Dar es Salaam kutimiza ahadi yake ya kuziunga mkono timu za Simba Sc na Yanga Sc zinazoshiriki mashindano ya Kimataifa.
Mapema wiki iliyopitaKanali Abbas aliahidi kutoa kiasi cha shilingi 1000,000/= kwa kila goli litakalofungwa na timu za YangaSc na Simba Sc zinazoshiriki mashindano ya Kimataifa ambapo Jumapili iliyopita Februari 19 Yanga Sc iliifunga TP Mazembe magoli 3 - 0.
Akikabidhi kitita cha shilingi 3,000,000/= kwa Rais wa Yanga Eng. Hersi Said kutimiza ahadi yake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema wanamtwara wote wanatambua na kuthamini kazi nzuri ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye usiku na mchana amekuwa mstari wa mbele kuziunga mkono sekta mbalimbali ikiwemo michezo na kuongeza kuwa ametoa motisha hiyo kama ishara ya kuunga mkono jitihada hizo.
"Sote tunatambua Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa kuhakikisha sekta zote ikiwemo michezo zinafanya vizuri, ndio maana sisi Mtwara tumeona tujitokeze kuunga mkono jitihada hizo tukiamini hatua hii itaongeza hamasa katika sekta ya michezo nchini" alisema Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Pia Kanali Abbas amemuomba Rais wa Yanga kuangalia uwezekano wa kuimarisha ushirikiano kati ya Klabu ya Yanga na Mkoa wa Mtwara ili kuinua sekta ya michezo sambamba na kuinua vipaji vipya.
Kwa upande wake Rais wa Club ya Yanga Eng. Hersi Said, baada ya kupokea motisha hiyo ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Mtwara kwa ubunifu huo na kuongeza kuwa Utamaduni huo utaongeza chachu ya ushindani miongoni mwa vilabu huku akiwataka wadau wengine wa soka kuiga mfano huo.
"Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza sana wewe Mhe. Mkuu wa Mkoa pamoja na timu yako kwa kuthamini mafanikio ya timu yetu ambayo juzi imepeperusha vema bendera yaTaifa " alisema Eng. Hersi.
Halikadhalika Eng. Hersi Said amemuahidi Mkuu wa Mkoa kuwa, club ya Yanga iko tayari kushirikiana na Mkoa wa Mtwara ambao ameutaja kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa nyingi za kiuchumi.
Eng. Hersi ameongeza kuwa kwa muda wa wiki moja kuanzia leo mitandao yote ya kijamii ya club ya Yanga itarusha habari zinazoutangaza Mkoa kama njia ya kudumisha ushirikiano.
Aidha Mkuu wa Mkoa Kanali Ahmed Abbas Ahmed amemuomba Eng. Hersi Said kupitia vyombo vya habari vya Yanga kuwahabarisha wananchi kuhusu shughuli ya Uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru utakaozinduliwa katika Uwanja wa Nangwanda Aprili 2 mwaka huu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.