Viongozi wa Taasisi Binafsi, Taasisi za Serikali, Viongozi wa Dini, pamoja na Mashirika ya Umma na binafsi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Selemani Mzee (hayupo Pichani) katika kikao kilicholenga kupeana maelekezo ya namna ya kupambana na ugonjwa wa COVID-19 unaosabishwa na virusi vya CORONA
Viongozi wa Serikali, Mashirika ya Dini, Taasisi za umma na binafsi Mkoani Mtwara wameshikamana pamoja kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha ili kujiepusha na ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.
Mshikamano huu ulioanza mara tu baada ya kuenea kwa taarifa za kuibuka kwa ugonjwa huo huko nchini China umepata nguzu zaidi baada ya taarifa ya kuwepo kwa mgonjwa wa aina hiyo huko Arusha. Taarifa ya kuwepo kwa mgonjwa wa COVID-19 ilitolewa jana Machi 16, 2020 na Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu akielezea kuwa mgonjwa huyo ambaye ni Mtanzania aliwasili mjini Arusha na ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda akitokea Ubelgiji.
Mwandishi wa habari hii amewashuhudia Maafisa wa Afya wa Sekretarieti ya Mkoa pamoja na wale wa Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa nyakati tofauti wakitoa elimu ya jinsi ugonjwa huo unavyoenezwa na namna ya kujikinga. Elimu hiyo imetolewa kupitia redio za mjini hapa ikiwemo radio Pride, Radio Safari pamoja na Jamii FM.
Afisa Afya Mkoa, Sasita Shabani Kupitia Radio Safari amewasisitiza wananchi kuwa ugonjwa wa COVID-19 unaenea kwa haraka sana na kwamba dalili za mgonjwa wa COVID-19 ni pamoja na homa kali ya mapafu, mafua, kikohozi na kuhema kwa shida. Amesisitiza wananchi kuhakikisha wanaosha mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka, kutumia vikinga pua na mdomo (Masks) hasa kwa wale wanaohudumia washukiwa wa Corona. Pia kuhakikisha wanaepuka mazingira ya kugusana kwani inarahisisha virusi hivyo kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Huko Mjini Masasi Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Selemani Mzee ameongoza kikao cha dharula cha Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ambacho vilevile kiliwashirikisha Viongozi wa Dini, Mashirika na Wadau mbalimbali. Pamoja na masuala mengine yanayohusiana na ugonjwa wa Corona, elimu ya jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo imetolewa.
Mheshiwa Mzee amesisitiza wenye nyumba za kulala wageni kuhakikisha wanawaandikisha wateja wao ili kuwa na takwimu sahihi ya wageni wanaoingia na kutoka.
Aidha amewataka Maafisa Watendaji wa vijiji vilivyoko katika mpaka wa wilaya yake na nchi jirani ya Msumbiji kuhakikisha wanatoa taarifa Juu ya wageni wanaoingia Nchini kupitia Maeneo yao. Ameendelea kuwasisitiza viongozi wa dini kuiombea nchi ili iepukane na gonjwa hili tayari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.