Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa akiwa na wanafunzi katika moja ya shule za Msingi Mkoani Mtwara
Jitihada kubwa ya uongozi wa mkoa wa Mtwara katika kuleta mageuzi chanya ya kieliu mkoani Mtwara zimeeanza kuzaa matunda mara baada ya Mkoa kutangazwa kuwa wa kwanza katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita 2018 Kitaifa. Kupitia matokeo hayo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa mwishoni mwa wiki Mkoa wa Mtwara wenye shule kumi na moja za kidato cha sita umeshika nafasi hiyo baada ya kuwezesha watahiniwa wote 1499 kufaulu.
Licha ya kutokuwepo kwa mwanafunzi aliyepata daraja sifuli katika mitihani hiyo iliyohusisha mikoa yote 29 ya Tanzania, ni watahiniwa kumi na moja tu kutoka mkoani Mtwara waliofaulu kwa daraja la Nne huku wengine wote 1488 wakiwa wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu.
Kwa ufaulu huu mzuri wadau wa maendeleo na elimu mkoani Mtwara wamepongeza uongozi wa mkoa chini ya Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Gelasius Byakanwa.
Godfrey Mwambe wa Ndanda Mtwara ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ameandika kwa kifupi kwenye kundi la whatasap la viongozi wa Mkoa wa Mtwara ‘Mtwara Leaders Group’.
“Hongera kwa uongozi wa Mkoa wa Mtwara, kwa Chama na Serikali kufanikisha mkoa wetu kuongoza kitaifa. Ni imani yangu kuwa Mikakati iliyofanikisha ufaulu huu itaimarishwa zaidi ili matokeo ya form IV na Standard VII yaakisi ufaulu huu. Hongera sana viongozi wetu Mtwara”.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mussa Chimaye anaandika katika ukurasa huo akikumbusha jithada kubwa zilizofanyika na wadau wa elimu mkoani hapa katika kuhakikisha ufaulu wa mkoa unapanda.
“Hongereni sana viongozi wetu, Mhe. RC na timu nzima ya RS kwa miongozo yenu na hatimaye tumekuwa wa kwanza kitaifa. Kumbe inawezekana”.
Naye Mzee Sallum Ahmad wa Mikindani Mtwara amepongeza ufaulu huo na kuwataka wadau wote wa elimu kushikilia kile walichokubaliana katika vikao mbalimbali vya kuinua elimu Mkoani.
Mwandishi wa Habari hii ameshuhudia maandalizi ya kikao maalumu cha Mkuu wa Mkoa na walimu wa sekondari mkoani hapa yakiendelea katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo mmoja wa waandaaji hao amesema ni kwa ajili ya Mheshimiwa Mkuu wa mkoa kutoa neno la shukrani kwa walimu na wadau wote waliofanikisha matokeo haya. Kikao hicho kimetajwa kufanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Aguinas iliyoko Mtwara Mjini.
Mapema mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa aliagiza kuhakikisha kila Mkurugenzi anaweka mikakati ya itakayoleta mabadiliko chanya katika ufaulu wa wanafunzi. Kupitia vikao vya wadau wa elimu alivyoviitisha kufuatia ufaulu duni wa matokeo ya kidato cha Nne mwaka 2017 ambapo mkoa ulishika nafasi ya 26 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara aliagiza muhtasari wa masomo kukamilika mwezi wa sita ili wanafunzi wapate muda mrefu wa kujisomea na kufanya mitihani ya majaribio.
Pia aliagiza kuwepo njia mbalimbali za kuwapa motisha wanafunzi na wadau wote wanaofanikisha ufaulu wa wanafunzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.